Gwambina yafufukia kwa Ihefu

Saturday October 03 2020
gwambina pic

Gwambina FC imepata ushindi wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga Ihefu Fc mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika leo mchana Oktoba 3 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Mabao ya Meshack Abraham dakika ya 33 na 48 yalitosha kuipa ushindi Gwambina ambayo tangu Ligi Kuu ianze msimu huu haikuwahi kuonja ladha ya ushindi.

Mabao ya mchezaji huyo pia yameifanya Gwambina kuondoka katika timu ambayo ilikuwa haijafunga bao lolote tangu msimu huu wa ligi uanze hivyo kuiacha Mbeya City pekee ambayo nayo ilikuwa uwanjani ikipambana na watani zao wa jadi Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

Ushindi huo unaweza kumuweka salama kocha wa Gwambina Fc, Fulgence Novatus ambaye amekalia kuti kavu kutokana na timu hiyo iliyopanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza mimu huu kuwa na matokeo mabaya mfululizo.

Habari zinadai kama kikosi hicho kingeendelea kupata matokeo mabaya basi nafasi ya Fulgence kuendelea kusalia ndani ya timu hiyo ingezidi kuwa finyu.

Advertisement