Gomes: Yanga? Subirini muone!

Muktasari:

KUMBE kelele za mashabiki wa Yanga kwamba msimu huu wana jambo lao, hasa kwa kukiangalia kikosi chao na kuona kimejaa majembe ya maana kupitia usajili uliofanywa na mabosi wao, ila kumbe hata Kocha wa Simba, Didier Gomes amezisikia na kutamka neno moja ambalo linaweza likawachanganya wanayanga.

CHARITY JAMES

KUMBE kelele za mashabiki wa Yanga kwamba msimu huu wana jambo lao, hasa kwa kukiangalia kikosi chao na kuona kimejaa majembe ya maana kupitia usajili uliofanywa na mabosi wao, ila kumbe hata Kocha wa Simba, Didier Gomes amezisikia na kutamka neno moja ambalo linaweza likawachanganya wanayanga.

Gomes amekiri ni kweli watani wao wamefanya usajili mzuri, lakini akasema hata wao wapo vizuri na kwamba kila mtu atavuna kile atakachopanda msimu huu hasa kutokana na udhamini mnono uliopo, huku akitangaza rasmi kuyazika mafaili ya nyota wake wa zamani, Luis Miquissone na Clatous Chama waliouzwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo anayeliandaa jeshi lake kwa ajili ya mechi za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, alisema anatarajia msimu mgumu tofauti na misimu minne iliyopita ambayo kwao alikuwa bora na kufanikiwa kubeba ubingwa na kutetea mara zote.

Msimu uliopita Simba ilitetea ubingwa wa ligi kwa mara ya nne mfululizo na kubeba pia Kombe la Shirikisho (ASFC) kwa mara ya pili mfululizo, huku kwa sasa baada ya ligi kupigwa mechi za raundi mbili, Simba imevuna alama nne tu, mbili pungufu na ilizonazo Yanga yenye pointi sita kama Polisi Tanzania.

Hata hivyo, Kocha Gomes alisema hatishwi na moto uliokuwepo kwenye ligi kwa sasa kwa vile ni mapema mno kuanza kutabiri, lakini alisema mwisho wa msimu kila kitu kitakuwa wazi.

“Ndani ya misimu minne Simba ndio timu iliyokuwa bora na ilithibitisha hilo kwa kutwaa mataji lakini msimu huu kazi ni kubwa ya kuhakikisha tunaendeleza ushindani kutokana na ukweli kikosi kina ingizo jipya,” alisema Gomes na kuongeza;

“Wapinzani wetu Yanga msimu huu wa utofauti mkubwa na misimu yetu bora minne iliyopita wamefanya usajili mzuri na mkubwa kutokana na hilo tunatarajia ushindani mkubwa na sio kutoka kwao tu na hata timu ndogo ambazo pia msimu huu zinaonekata kuhitaji fedha na taji.”

Mfaransa huyo alisisitiza licha ya ugumu huo anaouona ndani ya msimu huu na wapinzani walivyo kwa sasa, lakini kiu yao kama Simba ni kuona anaendeleza ubora wao kwa kutetea ubingwa na kufanya vizuri zaidi kwenye michuano mingine watakayoshiriki ili kuwapa raha mashabiki wao.

“Bado tunahitaji kuendeleza ubora wa kikosi ili kutetea mataji yetu sambamba na kukabiliana na changamoto ya kukitengeneza kikosi kadri mechi zinavyoendelea kuchezwa,” alisema Gomes aliyeifikisha Simba hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo msimu huu wameanzia raundi ya kwanza wakitarajia kuifuata Galaxy watakacheza nao Oktoba 17 kisha kurudiana nao wiki moja baadaye jijini Dar.


AZIKA FAILI LA LUIS, CHAMA

Akizungumzia juu ya kuondoka kwa nyota wake waliochangia mafanikio ya msimu wake wa kwanza Msimbazi, Luis Miquissone aliyeuzwa Al Ahly ya Misri na Clatous Chama anayekipiga kwa sasa RS Berkane ya Morocco, Gomes alisema baada ya kuuzwa kwa sasa hawana nafasi tena kwake na Simba kwa ujumla.

Gomes alisema wachezaji wapya na wale waliosalia kikosi kutoka msimu uliopita ni bora na wenye kuweza kuibeba timu, kitu ambacho kinamfanya ajiamini na kusahau kila kitu kuhusu kina Luis, licha ya ukweli walipokuwa Simba walikuwa ni tegemeo.

“Nawashangaa sana wadau na mashabiki kuendelea kuwataja Luis na Chama wakati hawapo sasa tuna wachezaji wapya na wao pia wana uwezo japo wanahitaji muda ili kuingia kwenye mfumo hao wanaowataja sasa walipokuwa wanaingia mara ya kwanza Simba hawakuwa na ubora huo walioondoka nao,” alisema Gomes na kuongeza;

“Kila mchezaji ana aina yake ya uchezaji na ana umuhimu wake, pia kina Luis walikuwepo walicheza vizuri na sasa wameondoka. Kuondoka kwao sio kwamba wameondoka na timu wameiacha na itaendelea kufanya vizuri kwani imesajili mbadala wao na sasa tunahitaji kuwapa muda na kuwaamini na bila shaka wataleta matokeo chanya.”