Giniki, Angelina wafunika Lake Victoria Marathon 2024

Muktasari:
- Muktasari: Wanariadha Shing’ade Giniki na Angelina John wameshinda mbio za Lake Victoria Marathon zilizoshirikisha zaidi ya wanariadha 500 kutoka mikoa mbalimbali nchini zikiwa na lengo la kuvutia utalii na kustiri watoto wa kike kwa kuwanunulia taulo za kike
WANARIADHA Shing’ade Giniki na Angelina John wameibuka washindi wa mbio za Lake Victoria Marathon 2024 zilizofanyika leo Jumapili Julai 7, 2024 kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini hapa zikishirikisha wanariadha kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Giniki ambaye msimu uliopita alimaliza wa pili, amekuwa mshindi wa kwanza kwa wavulana Kilometa 21 katika mbio hizo zilizoanza saa 12 asubuhi kwenye Uwanja wa Nyamagana na kumalizika saa 3 asubuhi uwanjani hapo na kujinyakulia Sh1 milioni.
Rashid Omary kutoka Singida ameibuka mshindi wa pili na kunyakua Sh750,000, Isack Benjamin (Arusha) mshindi wa tatu akipata Sh500,000, Jamal Said (Arusha) mshindi wa nne akipata Sh350,000 huku Jonas John kutoka Singida akiambulia Sh150,000 baada ya kumaliza wa tano.
Kwa upande wa wasichana kilometa 21, Angelina John kutoka Singida ameibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia Sh1 milioni, Tunu Andrea (Singida) mshindi wa pili (Sh750,000), Edista Iddi (Singida) mshindi wa tatu akipata Sh500,000, Hellen Mosha (Mwanza) mshindi wa nne (Sh350,000) na Navelina Tarimo wa Mwanza akimaliza wa tano na kupata Sh150,000.
Katika mbio za kilomita 10, Neema Festo wa Arusha amekuwa mshindi wa kwanza kwa upande wa wasichana na kupata Sh1 milioni, Warda Shaban wa Singida akishika nafasi ya pili na kupata Sh500,000, Neema Sanka wa Manyara akiibuka wa tatu, Abishagi Bhoke (Mwanza) nafasi ya nne na Magdalena Shiluba (Shinyanga) wa tano.
Dickson Paul wa Mwanza ameibuka wa kwanza kwa upande wa wavulana na kuzawadiwa Sh750,000, huku washindi wengine wakiwekwa kando kutokana na udanganyifu. Mbio hizo pia zilikuwa na kipengele cha Kilomita tano zilizoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda huku Hija Juma wa Geita akiibuka mshindi wa kwanza kwa watoto Kilomita 2.5.
Akizungumzia ushindi huo, Giniki amesema siri ya mafanikio hayo ni maandalizi mazuri ya mazoezi na kujituma baada ya msimu uliopita kushika nafasi ya pili, huku akisisitiza kwamba mbio ni ajira kwa watu wengi licha ya wengine kuzitumia kuimarisha afya kwa kufanya mazoezi.
"Mashindano yanahitaji mazoezi na maandalizi mazuri na kuwa nidhamu ya kumsikiliza kocha. Nidhamu ndiyo inamtengeneza mchezaji kuwa imara, japokuwa bado tunapata changamoto ya ukosefu wa vifaa bora lakini mbio hizi zimekuwa na maandalizi mazuri," amesema Giniki.
Tunu Andrea aliyeshika nafasi ya pili kilomita 21 kwa wasichana amesema; "Nilijiandaa kuwa mshindi wa kwanza lakini nashukuru kwa nilichokipata kwa sababu mwaka juzi pia niliishia nafasi ya pili, tunaomba mashindano kama haya yawepo mengi na yafanyike mara kwa mara wanariadha wapate jukwaa la kuonekana."
Mratibu wa mbio hizo, Hilda Vigo amesema msimu huu ambao ni wa nne umeshirikisha zaidi ya wanariadha 500 kutoka mikoa mbalimbali zikilenga kukusanya fedha za kusaidia kutoa taulo za kike na kutoa elimu kwa watoto wa kike, huku watoto 78 wakishiriki mbio za kilomita 2.5.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema; "Mbio hizi zimekuwa chachu ya kuvutia na kuongeza watalii wa ndani na nje kwenye maeneo na vivutio vya utalii, nitumie fursa hii kuwaalika Watanzania kuja Mwanza kujionea utalii wa vitu mbalimbali kwa sababu Mwanza ni kitovu cha michezo.”