Geita hali mbaya, Matampi vitani na Diarra

Muktasari:

  • Katika mchezo huo imeshuhudiwa kipa wa Coastal Union, Ley Matampi akiondoka na clean sheet ikiwa ya 13 kwake ndani ya ligi hiyo msimu huu na kumfikia Djigui Diara wa Yanga.

GEITA Gold imeendelea kuwa na hali mbaya katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya jioni ya leo kutoka suluhu dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa ligi hiyo uliochezwa Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita.

Katika mchezo huo imeshuhudiwa kipa wa Coastal Union, Ley Matampi akiondoka na clean sheet ikiwa ya 13 kwake ndani ya ligi hiyo msimu huu na kumfikia Djigui Diara wa Yanga.

Dakika 90 za mchezo huo zilikuwa na ushindani wa aina yake ambapo Geita iliingia kwa kushambulia dakika zote ikiwatumia zaidi mawinga wake lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Coastal Union ikiongozwa na Lameck Lawi uliwanyima upenyo timu hiyo kupata bao.

Mbali na mabeki wa Coastal kuwa bora lakini kipa wa timu hiyo Matampi ameendelea kuwa bora zaidi baada ya kuokoa mipira ya hatari iliyokuwa inalenga lango lake.

Suluhu hiyo ya leo inamaanisha kwamba Coastal Union imefikisha pointi 38 ikiendelea kujiimarisha hapo ikiwa imebakiwa na michezo mitatu mkononi yenye pointi tisa ambapo wakikusanya saba pekee watakuwa na uhakika wa kumaliza hapo kwani pointi 45 hazitaweza kufikiwa na walio chini yake.

Kwa upande wa Geita Gold, suluhu hiyo ya nyumbani inawafanya kuendelea kusalia nafasi ya 15 kwa kukusanya pointi 25 ikiizidi Mtibwa Sugar iliyo mkiani kabisa pointi tano pekee huku zote zikibakiwa na mechi tatu za kuamua hatma yao.

Kama Geita ingepata ushindi kwenye mchezo huo ingejinasua kutoka nafasi ya 15 hadi ya 13 na kukwepa mtego wa kushuka daraja huku Coastal yenyewe ingeshinda basi ingekuwa karibu zaidi kujihakikishia nafasi ya nne kwani ingefikisha pointi 40.

Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika, Kocha wa Geita, Denis Kitambi alisema walitengeneza nafasi nyingi lakini tatizo lilikuwa kwenye umaliziaji ambao umewanyima pointi tatu.

"Tatizo letu hatukuingiza mpira nyavuni, tupo kwenye nfasi ngumu tutajitahidi tupambane mechi tatu zilizosalia na hazitakuwa rahisi kwani mechi ijayo tutakuwa ugenini dhidi ya Simba," alisema Kitambi.

Kocha Mkuu wa Coastal Union, David Ouma alisema walijua Geita wameingia na mpango gani hivyo wakachezesha mabeki watatu kwa lengo la kulinda na kuishinda mipira mirefu.

"Licha kwamba tumegawana pointi lakini Geita imetupa wakati mgumu, nawapongeza, tulijua mpango wao kwa kuwa walikuwa wanahitaji pointi tatu wangeweza kuwatumia mawinga wao na sisi tukawabana ili wasipige krosi zitakazotuathiri baadae." 

Geita Gold imebakiwa na mechi tatu za kuamua hatma yao ya kusalia ligi kuu ambapo itacheza dhidi ya Simba (Mei 21 ugenini), Singida Fountain Gate (Mei 25 ugenini) na Azam (Mei 28 nyumbani).

Coastal Union yenyewe katika mechi tatu zilizobaki itacheza dhidi ya Kagera Sugar (Mei 25 ugenini), JKT Tanzania (Mei 25 nyumbani) na KMC (Mei 28 nyumbani).