Gamondi: Tumeshajua dawa yao

BAADA ya kikosi cha Yanga kuendeleza rekodi yake ya kushinda mabao mengi kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi ametoa siri na mipango mizito waliyo nayo katika Ligi ya Mabingwa.
Rekodi hizo zimeendelea kuifanya Yanga kuwa tishio hasa inapocheza na timu zingine zilizopo chini yake katika msimamo wa ligi kutokana na ubora waliokuwa nao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi ameeleza kuwa, wao kufanya vizuri sio rahisi kama inavyoonekana ila wamegundua namna ya kucheza na timu zote zinazokuja mbele yao.
Ameeleza kuwa Ihefu ilikuja kwa njia ya kuzuia na sio kushambulia ili kupata matokeo kama wengi walivyodhani, lakini waliwasoma mapema na kutafuta namna ya kuvunja ukuta na kuwafunga.
"Nafurahia ubora wa wachezaji wangu na mpango wetu ni kuchukua ubingwa hadi wa Ligi ya Mabingwa, kwani uwezo huo tunao na njaa ya matokeo ipo kwenye moyo wa kila mmoja wetu," amesema.
"Sasa tuna dawa ya kila aina ya mbinu watakazokuja nazo wapinzani wetu, hivyo hofu ya kufungwa haipo kwa wachezaji wangu kwani kila mchezo tunaoingia kucheza tunataka matokeo tu."
Kocha huyo ambaye ameanza kuifundisha Yanga msimu huu, amekuwa mwenye bahati kwani kikosi hicho kimekuwa na rekodi ya kuzibamiza mabao matano matano timu nane ndani ya msimu mmoja.
Yanga mpaka sasa katika Ligi Kuu imeshazifunga timu nne mabao matano katika ikiwemo watani wao Simba, JKT Tanzania, Ihefu na KMC, huku katika michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ni Polisi Tanzania na Hausung ilhali katika hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika ni Asas FC ya Djibout.
Yanga inayoongoza ligi ikiwa na alama 49 itakuwa nyumbani ikiikaribisha Geita Gold keshokutwa, Machi 14, huku rekodi zikionyesha katika mchezo wa mwisho ambapo Geita ilikuwa wenyeji ilifungwa mabao 3-0.