Gamondi: Aucho bado, atamba kubeba makombe

Muktasari:

  • Khalid Aucho amekosekana kwa takribani mwezi mmoja akiuguza majeraha ya goti, huku Pacome Zouzoua akiwa na maumivu ya enka na Yao Kouassi akikabiliwa na majeraha ya kuchanika nyama za paja.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema mazoezi ya mwisho leo jijini Mwanza yataamua hatma ya kiungo, Khalid Aucho kama atatumika katika mchezo wa kesho ama la licha ya kucheza kwa dakika chache m chezo wa FA dhidi ya Dodoma Jiji, huku akitamba kuwa kukosekana kwa mchezaji yeyote kikosini kwake siyo tatizo kwani timu hiyo imejengwa kwa umoja bila kumtegemea mtu mmoja.

Yanga itakuwa mgeni wa Singida Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kesho Aprili 14 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni, huku ikihitaji ushindi ili kuendelea kuwa juu ya msimamo wa ligi hiyo.

Aucho ambaye amekuwa nguzo muhimu katika kuilinda safu ya ulinzi ya Yanga amekosekana kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja akipatiwa matibabu ya goti, huku pia ikiwakosa Pacome Zouzoua anayekabiliwa na majeraha ya enka huku beki wa pembeni, Kouassi Attohoula akiuguza majeraha ya kuchanika nyama za paja.

Akizungumza leo Aprili 13, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza, Gamondi amesema kupitia mazoezi ya mwisho ambayo yatafanyika leo jioni watapata uhakika wachezaji gani watapatikana kwa mechi ya kesho.

Muargentina huyo amesema bado kikosi chake hakijapata muda wa kutosha wa kufanya maandalizi makubwa kwa ajili ya mechi zinazowakabili kutokana na ufinyu wa muda ambapo timu hiyo ilitua jana usiku jijini hapa.

"Tunacheza vizuri na tunaendelea kucheza katika namna ambayo tumekuwa tulicheza, Khalid ni kama amepona kabisa ila hana utimamu wa kucheza kwa asilimia 100 lakini anaweza kutumika kwa dakika 25 kesho, labda anaweza kuanza na kucheza kwa dakika kadhaa tutaona," amesema Gamondi na kuongeza;

"Kwetu sisi kitu cha muhimu ni timu, ni kweli kuna wachezaji wamekuwa na mchango muhimu katika timu lakini tulicheza mechi ngumu ya Ligi ya Mabingwa bila baadhi ya wachezaji na tukaonyesha ubora, kwahiyo siyo kazi ya mtu mmoja ni timu.

"Nafikiri moja ya nguzo ya Yanga ni hiyo kwamba tunafanya kazi kama timu, tunapambana na pale baadhi ya wachezaji wanapokosekana anapatikana mwingine anayeweza kuziba nafasi na akafanya vizuri kama ilivyokuwa kwenye nafasi za Pacome, Aucho na Yao," amesema Gamondi.

Gamondi alisema wanatarajia mchezo wa kesho dhidi ya Singida Fountain Gate utakuwa mgumu kwakuwa wao ni vinara wa ligi na timu nyingi zimekuwa zikiwapa upinzani mkubwa, huku akitahadharisha kwamba matokeo mabovu waliyonayo Singida hayatawafanya waende kinyonge kwani wanahitaji ushindi ili kuendelea kuongoza ligi.

"Tunahitaji kufanya kila liwezekano kushinda mataji yote ambayo tumebakiza. Yanga inahitaji kushinda na mimi kama kocha naamini katika hatua, kila mchezo na kesho tunahitaji ushindi ili kwenda mbele zaidi," amesema.

Beki wa timu hiyo, Gift Fredy, amesema: "tumejiandaa vizuri ili kuendelea kuwafurahisha mashabiki wetu ili mwisho wa msimu tuwe mabingwa. Ni sehemu ya mchezaji unapopewa nafasi uonyeshe, Yanga ni timu kubwa yenye wachezaji wazuri siyo rahisi kupata nafasi ya kuanza hivyo kila mmoja anajituma kuhakikisha anaisaidia timu."