Gamondi apiga mkwara mpya kambini Yanga SC

Muktasari:

  • Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba, Jumamosi Aprili 20, mwaka huu, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, mechi ambayo kwa namna yoyote inakuwa na presha kubwa ndani na nje ya uwanja. Simba wao wamejificha Zanzibar.

Yanga imeingia kambini jana tayari kwa maandalizi yao ya kuwakaribisha watani wao Simba, lakini kuna mkwara mzito wameshushiwa mastaa wao kisa Wekundu hao.

Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba, Jumamosi Aprili 20, mwaka huu, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, mechi ambayo kwa namna yoyote inakuwa na presha kubwa ndani na nje ya uwanja. Simba wao wamejificha Zanzibar.

Wakati Yanga ikiingia kambini jana, mastaa wake wakakutana na mkwara mzito kwenye kikao dhidi ya viongozi wao wa juu, waiambiwa hawatakiwi kabisa kuchukua makelele ya mashabiki kuwa watani wao kikosi chao ni dhaifu na kinafungika kirahisi.

Mwanaspoti linajua kikao hicho kilichofanyika kambini kiliongozwa na Rais wa klabu hiyo, Hersi Said na hata kocha wao, Miguel Gamondi alikazia. Habari zinasema katika kikao hicho cha siri Wachezaji waliambiwa,  wanatakiwa kujiandaa na dakika 90 ngumu mbele ya watani wao ambazo huenda zikawa na sapraizi kuliko wanavyodhania hivyo wasiende na upepo wa kishabiki.

“Tumewaambia kwamba wanatakiwa kuachana na makelele ya mashabiki, kwani wachezaji kazi yao ni kwenda kuutafuta ushindi kwa kucheza bila dharau na kuipigania timu uwanjani kwa umakini mkubwa, wakati mashabiki kazi yao ni kupiga kelele majukwaani,”alidokeza bosi mmoja aliyekuwa kwenye kikao hicho kilichotoka na mkakati kwamba Jumamosi ni fainali ya Ubingwa wao.

Mapema Kocha Gamondi aliliambia Mwanaspoti kuwa, wao hawawezi kuwa na akili za mashabiki wao kwa kuona kama mchezo huo ni rahisi na kwamba wataifunga Simba kirahisi.

Gamondi alisema Yanga itakwenda kutafuta ushindi kwa akili na maarifa makubwa wakitumia falsafa yao kama ambavyo walivyofanya kwenye mechi zingine.

“Sisi sio mashabiki, sisi ni profeshno, hatuwezi kufanya makosa hayo, tumeshinda mechi hizi zote kwa kutanguliza weledi kwa kuwaheshimu kwanza wapinzani wetu bila kujali changamoto zao,” alisema Gamondi na kuongeza.

“Tunauhitaji ushindi huu kama ambavyo tumekuwa tukihitaji kushinda mechi zilizopita, tutakwenda kucheza mechi hii bila presha kwa kutumia falsafa yetu kuweza kushinda mechi hii na haitakuwa rahisi kabisa.”

Hii inakuwa ni mechi ya tatu kwa Gamondi dhidi ya Simba msimu huu ukiwa ni wa kwanza kwake akiwa Yanga, alikutana na Wekundu hao katika Ngao ya Jamii, akapoteza kwa penalti, kisha akashinda 5-1 ndani ya ligi wakati timu hiyo ikiwa chini ya Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’. Hivi sasa anakwenda kukutana na Simba ikiongozwa na Kocha Abdelhak Benchikha.