Gamondi aibua shangwe lingine Yanga

Muktasari:

  • Yanga imepitisha bajeti ya msimu mpya wa mashindano ya Sh 24.5 bilioni, ikiwa ni zaidi ya ile iliyotumika msimu huu iliyokuwa ya Sh 21 ambapo iliiwezesha timu hiyo kushusha majembe ya maana kama Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Yao Kouassi na kutetea mataji mawili ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kwa msimu wa tatu mfululizo na kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa baada ya miaka 25 na kufika robo fainali.

KILICHOFANYWA na Yanga jana katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo ni kama imewatangazia wapinzani kuwa, ile tabu waliyokutana nayo msimu wa 2023-2024 wasidhani imesha badala yaje wajue  mapema bado ipo palepale baada ya kupitisha bajeti ya kibabe huku ikimuongezea mkataba mpya kocha Miguel Gamondi.

Yanga imepitisha bajeti ya msimu mpya wa mashindano ya Sh 24.5 bilioni, ikiwa ni zaidi ya ile iliyotumika msimu huu iliyokuwa ya Sh 21 ambapo iliiwezesha timu hiyo kushusha majembe ya maana kama Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Yao Kouassi na kutetea mataji mawili ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kwa msimu wa tatu mfululizo na kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa baada ya miaka 25 na kufika robo fainali.

Utamu zaidi ni kwamba kocha aliyeiwezesha Yanga kufikia mafanikio hayo ikiwamo kugawa dozi nene kwa wapinzani ikiwamo kuwafumua Simba kwa jumla ya mabao 7-2 katika Dabi ya Kariakoo, haondoki tena baada ya mabosi wa klabu hiyo kutangaza kumuongezea mkataba mpya ili aendelee pale alipoishia.

Gamondi aliyekuwa amemaliza mkataba na kuzua sintofahamu kwamba kwamba huenda akatimka klabu kutokana na kuwa ofa kadhaa mezani, aliibukia kwenye ukumbi wa mkutano kama sapraizi ambayo Gazeti la Mwanaspoti liliwadokeza jana kisha Rais wa Yanga, Hersi Said alisema wamempa mwaka mmoja mwingine.

Katika kusindikiza sapraizi hiyo iliyoambatana na kocha huyo kusisitiza bado yupo kumalizia kazi aliyoianza, kulikuwa na kichombezo cha ujumbe unasomeka kwenye skrini kwamba ‘Tabu bado ipo palepale’ ikiwa na maana zile dozi za Gamondi na Yanga kutawala soka la Tanzania itaendelea na wajumbe kushangweka.

Chini ya Gamondi, Yanga iliweza kulipa kisasi kwa kuifunga Simba mabao 5-1 zilipokutana Novemba 5 mwaka jana, ikiwa ni wiki kadhaa tangu ilipozinyoosha Asas ya Djibouti, JKT Tanzania na KMC na baada ya hapo ikazinyoosha tena Hausing, Polisi Tanzania, Jamhuri na kumalizia na Ihefu zilizokuwa kati ya mabao 5-0 na 5-1 na kutetea mataji ya iliyokuwa ikiyashikilia, huku CAF ikifika robo fainali baada ya miaka mingi.


NDUMBARO AUKUBALI MZIKI

Katika mkutano huo,  uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere uliopo Posta jijini Dar es Salaam, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro alikiri Yanga ya sasa ni moto na kuipongeza kwa mafanikio iliyopata msimu uliopita na ule uliomalizika hivi karibuni akisema kama sio mizengwe ya soka Afrika, timu hiyo ingekuwa ya kwanza kuleta mataji ya CAF nchini.

Dk Ndumbaro anyefahamika kuwa ni Mnyama sana, alisema kinachotokea katika klabu hiyo ya Msimbazi sio kama imeshuka viwango, bali ubora wa Yanga na Azam ndio unawafanya waruhusu migogoro na kupagawa.

“Shida ya Simba ni kupanda kiwango kwa timu pinzani hasa Yanga na Azam, ubora wa hizi timu mbili ndio unayoifanya Simba ionekane iko chini. Nawapongeza sana Yanga mnaendelea kufanya vizuri shida ya hizi klabu mbili hii ikishuka na nyingine inapiga hatua, mkishuka kaeni chini mjijenge upya mpate  maendeleo.”


BAJETI NA HASARA

Katika mkutano huo ulioanza saa 4 kasorobo ukiwa na ajenda 10, Yanga iliweka bayana imepata hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni kwa mujibu wa ripoti ya mapato na matumizi kwa msimu wa 2023/2024.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa wajumbe ilionyesha kwamba Yanga ilipata mapato ya jumla ya Sh21.19 bilioni, lakini matumizi yalikuwa ni Sh.22.29, hivyo kuingiza hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni.

Usajili na uhamisho wa mastaa kama kina Pacome Zouzoua, Yao Kouassi, Joseph Guede ni moja ya maeneo yaliyotumia fedha nyingi, ambapo Sh3.5 bilioni zilitumika kuhakikisha klabu inapata wachezaji bora. Gharama za mishahara kwa wachezaji na benchi la ufundi zilitumia sehemu kubwa zaidi ya bajeti, ikifikia Sh7.39 bilioni. Hii inaonyesha nia ya klabu kuboresha viwango vya wachezaji na kuhakikisha wanapata maslahi bora.

Matumizi mengine muhimu ni pamoja na usafiri, chakula na malazi, ambapo klabu ilitumia Sh 2.89 bilioni kuhakikisha wachezaji na benchi la ufundi wanapata huduma bora wakati wa safari na kambi za mazoezi. Maandalizi ya mechi nayo yaligharimu Sh 1.85 bilioni, fedha hizi zikiwa zimeelekezwa katika kuhakikisha vifaa na maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mechi yanakamilika kwa wakati.

Motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi imechukua Sh 2.6 bilioni, fedha hizi zikiwa ni kwa ajili ya bonasi na zawadi kwa wachezaji na makocha kutokana na mafanikio mbalimbali. Gharama za kambi zimesimama kwenye Sh702 milioni, huku ‘compliance’ ikigharimu Sh944 milioni. Gharama za kiutawala zimefikia Sh 1.46 bilioni, ikijumuisha matumizi ya ofisi na mishahara ya wafanyakazi wa utawala.

Aidha, Yanga imetumia Sh424 milioni kwa ajili ya masoko na Sh503 milioni kwa gharama za kifedha, ambazo ni pamoja na riba za mikopo na huduma za kibenki. Jumla ya matumizi yote kwa msimu huu yamefikia Sh22.29 bilioni.

Ripoti hii inaonyesha jinsi klabu imekuwa ikijitahidi kuboresha miundombinu na ustawi wa wachezaji wake kupitia matumizi bora ya fedha. Kwa uwazi huu, Yanga SC inatarajia kuendelea kupata uungwaji mkono kutoka kwa wanachama na wadau mbalimbali ili kuleta mafanikio zaidi katika msimu ujao.

Yanga pia imetangaza bajeti ya timu hiyo ya Sh24.5 bilioni kwa msimu ujao wa mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi iliyopitishwa bila kupigwa na wajumbe wa mkutano huo uliohudhuriwa na vigogo wa serikali, Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa klabu na wadhamini wa klabu hiyo kwa ujumla.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Fedha, Sabri Sadick alisema ongezeko hilo ni kubwa zaidi ya msimu uliopita ila kukidhi mahitaji ya kikosi hicho.i.

Ongezeko hilo la bajeti kwa msimu ujao ni tofauti na ya msimu uliopita kwani klabu hiyo ilikuwa imetenga kiasi cha Sh20.8 bilioni katika Mkutano Mkuu uliofanyika Juni 24, mwaka jana.


HALI ILIVYOKUWA

Mkutano huo wa Yanga  umefanyika kwa viwango vikubwa vya weledi ndani yake wanachama wakitoka na tabasamu wakiamini kwamba furaha yao itaendelea zaidi.

Licha ya wanachama kuchelewa kujaa ukumbini hali iliyochelewesha mkutano kuchelewa kuanza, lakini baadaye mambo yalikaa sawa.

Yanga ilipanga kuanza mkutano huo saa 4:00 asubuhi lakini baadaye ukaanza 4:56, baada ya akidi kutimia kwa kujitokeza wanachama 526 kutimiza akidi kutoka wanachama 630 waliotakiwa kuhudhuria mkutano huo kutoka matawi 126.

Kila tawi lilitakiwa kutoa Wawakilishi watano ambao ndio Mabingwa wajumbe wa mkutano mkuu wa klabu hiyo.


MKUCHIKA v FEI TOTO

Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini la Yanga Kapteni mstaafu George Mkuchika ndiye aliyeanza kutoa neno kwenye mkutano huo ambapo ndani ya hotuba yake mbali na kuonyesha kuvutiwa na hatua ya timu yao kuchukua makombe mawili, alirusha kijembe kwa kiungo wa Azam Feisal Salum ‘Fei Toto’ kufuatia tukio la kuwanyamazisha mashabiki wa kikosi chao kwenye mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

“Kwenye mechi ile ya Fainali wakati timu yetu inapambana kwenye matuta, Kuna kijana mmoja akaonyesha ishara Mona hivi lakini wanajeshi wetu wakamtuliza wakapindua meza na kushinda kibabe, kwa kweli tunajivunia sana timu yetu kwa mafanikio haya,”alisema Mkuchika huku akishangiliwa na Ukumbi mzima.


SALAMU ZA WADHAMINI

Ndani ya mkutano huo wanachama walipokea salamu kutoka kwa wadhamini wao baadhi Saba tofauti kwa video zao kuonyeshwa ndani ya Ukumbi wakitoa pongezi zao kwa uongozi na kikosi hicho.


7-2 ZA SIMBA

Utani wa jadi uliendelea ndani ya ukumbi huo ambapo baada ya Yanga kuifunga watani wao Simba ndani nje, mabao yao Saba yalionyeshwa ndani ya Ukumbi na kuwafanya wajumbe kuishangilia wakati wote.

Kabla ya tano hizo kutajwa mapema serikali kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo iliwakilishwa awali na Katibu Mkuu Greyson Msigwa ambaye kwenye salamu zake aliwaasa Yanga kuhakikisha wanaendelea kupiga hatua na kuzitaka klabu zingine kuacha malumbano.

Hata hivyo, Msemaji wa Yanga Ally Kamwe alisherehesha kauli hiyo akidai wao Yangawala hawana shida na vurugu za wekundu hao na kwamba kwao watachekelea kama watani wao wataendelea kuvurugana.


UWANJA FRESHI

Mgeni rasmi kwenye mkutano huo alikuwa Waziri Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (Tamisemi) Mohamed Mchengerwa, kuwa ofisi yake imepokea maombi hayo na yataingizwa kwenye  wa uendelezaji wa mji katika Bonde la Mto Msimbazi.

Mchengerwa alisema,hivi karibuni atawakutanisha viongozi wa Yanga na ofisi inayoshughulikia mradi huo kuanza utekelezaji   wa kupatiwa eneo hilo kwa namna itakavyowezekana.

Aidha Mchengerwa aliwaonya Yanga kuhakikisha wanazingatia muda wa ujenzi wa Uwanja huo ambapo kama watazembea au kuharibu serikali haitasita kuwapokonya eneo hilo.

“Nataka kuweka wazi nitawafuatilia, mnanijua na wala sitaki kuwaficha, msipojenga kwa wakati na kufanya vizuri tutawapokonya hili niwasisitizie,” alisema Mchengerwa ambaye ni Mbunge wa Rufiji.


HERSI ATAMBIA USAJILI

Rais wa Yanga injinia Hersi Said kwenye hotuba yake, alisema baada ya mafanikio ya msimu uliomalizika, uongozi wao ukishirikiana na wadhamini wataendelea kuiboresha timu yao kwa kufanya usajili mzito utakaowafanya kuendeleza mafanikio yao kwa msimu ujao.

“Tutafanya usajili mkubwa na mzito, tutafanya maandalizi makubwa (pre season), tuna mialiko ya Kaizer Chiefs kwenda Afrika Kusini lakini pia tumealikwa na Raila Odinga Kenya ambako tunaweza kwenda kucheza dhidi ya klabu kubwa ya Ulaya, tunataka kuendelea kupata mafanikio zaidi kwa msimu ujao.”

Pia Hersi aliitambulisha kamati maalumu ya Mabadiliko ya Yanga inayoongozwa na Mwanasheria, Dk Alex Mgongolwa iliyoweka bayana kinachoendelea kuiweka klabu katoka mfumo wa kisasa wa kuendeshw akwa hisa.

Kamati hiyo ya mfumo wa mabadiliko Yanga pia ina wajumbe kama Eliakim Maswi, Raymond Wawa na Ivan Tarimo na Mgongolwa alisema;

“Mthamini ataitathini  klabu yetu  na kuona inathamani kiasi gani ili  kuifikisha katika soko la hisa,  matangazo yalitolewa katika vyombo vya magazeti. Tumepata makampuni zaidi ya 20, vigezo muhimu tutatazama kuwa hizo kampuni zimefanya kazi kwa muda gani, utaratibu gani utatumika katika kufanya tathimini. Sisi tuna mashabiki wengi hivyo nao ni thamani, uzoefu kiasi gani katika utendaji, muda je watafanya kazi kwa muda gani na itakuwa kwa kiasi gani.”

Licha ya makapuni mengi kutuma maombi ya tenda hiyo, mwanasheria huyo alisema watachagua tatu kabla ya kupata moja ambayo italibeba jambo hilo na Hersi Said aliongeza uala la mabadiliko wao watakuwa mashuhuda tu na kazi kubwa ikiachiwa kamati hiyo kuifikisha kula Yanga inakokutaka.

Na ilipofika saa 9154 alasiri mara baada ya sapraizi ya Gamondi mkutano ulifungwa na Hersi kisha wanachama na wajumbe wakaenda kupata chakula cha mchana ulioandaliwa na kumalizia kwa kupata posho za mkutano.