Fundi anatua Yanga

Muktasari:

SASA ni rasmi kwamba Yanga imebadili gia juu kwa juu kwa kuamua kuachana na Mfaransa Hubert Velud na kwenda na Sebastian Migne. Mwanaspoti limejiridhisha kwamba ilikuwa kwenye hatua za mwisho kabisa kumshusha Velud, lakini akataka vitu vikubwa kuliko bajeti na uwezo wa klabu. Migne analifahamu soka la Afrika na aliwahi kuifundisha Kenya ya staa Victor Wanyama kabla ya kuachana nayo.

SASA ni rasmi kwamba Yanga imebadili gia juu kwa juu kwa kuamua kuachana na Mfaransa Hubert Velud na kwenda na Sebastian Migne. Mwanaspoti limejiridhisha kwamba ilikuwa kwenye hatua za mwisho kabisa kumshusha Velud, lakini akataka vitu vikubwa kuliko bajeti na uwezo wa klabu. Migne analifahamu soka la Afrika na aliwahi kuifundisha Kenya ya staa Victor Wanyama kabla ya kuachana nayo.

Miongoni mwa timu alizowahi kufundisha Afrika ni timu ya vijana na wakubwa za DR Congo, Kenya na baadaye Guinea ya Ikweta.

Migne ambaye amebakiza siku kadhaa tu kutua nchini kuja kuchukua nafasi ya Mrundi Cedric Kaze, Yanga wanaamini anawabeba kutokana na uzoefu wake barani Afrika pamoja na soka lake la pasi za kuvutia na kwamba, pia ni muumini mkubwa wa nidhamu.

Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 48 alitema kibarua chake kuiona Equatorial Guinea mwishoni mwa mwaka jana kutokana na janga la corona ambapo mazingira yalikuwa magumu kwenye utendaji pamoja na kuwa mbali na familia yake iliyokuwa nchini Kenya.

Mara ya mwisho Migne kufanya kazi Afrika Mashariki ni pale alipoiongoza Kenya kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika nchini Misri, huku nahodha wa kikosi hicho cha Harambee akiwa kiungo Victor Wanyama.

Ingawa mabosi wa Yanga wakishirikiana na wadhamini wao walikubaliana kwamba kocha mzawa, Juma Mwambusi, apewe timu kwa muda, lakini inaelezwa kwamba wameamua kubadili gia angani kumshusha Migne haraka kuja kuungana na Mwambusi.

Mwanaspoti linafahamu kwamba chaguo la kwanza la mabosi wa juu wa Yanga lilikuwa kumchukua Velud ambaye kwa sasa anainoa Sudan, lakini dili hilo wameamua kuachana nalo ghafla na kumalizana na Migne.

Kocha huyo wa zamani wa TP Mazembe, taarifa za uhakika zinasema kwamba Yanga wameamua kumpiga chini kutokana na kushinikiza kulipwa mshahara wa zaidi ya Sh50milioni kwa mwezi huku ikiwa ni kinyume na bajeti ya Yanga.

Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Dominic Albinius aliliambia Mwanaspoti kwamba katika uamuzi wao wa kumpa timu Mwambusi haukatishi mawindo yao ya kusaka kocha mpya.

“Bado tutaendelea na mchakato wa kutafuta kocha mpya wakati huu timu tukimkabidhi Mwambusi tunachotaka ni kupata kocha sahihi ambaye atakuja kuendelea alipoishia Kaze,” alisema Albinius licha ya kwamba jana aligoma kuzungumzia wamefikia wapi.

“Tukimpata atakuja nchini na kuisoma timu wakati ikiwa chini ya Mwambusi atakachoweza kukifanya atakifanya wakishirikiana pamoja.” Yanga inaendelea na mazoezi makali Kigamboni jijini Dar es Salaam chini ya Mwambusi ambaye ni kocha wa zamani wa Mbeya City na Prisons anayesifika kwa matizi ya fiziki.