Fountain yazoa noti uhamisho wa Ubamba
Muktasari:
- Ubamba aliitumikia FC Masar inayoshiriki Ligi Kuu Soka Wanawake Misri kwa misimu miwili baada ya kuuzwa na Fountain Gate Princess mwaka 2024 kwa mkataba wa miaka mitatu ambapo umebaki mwaka mmoja ndipo akauzwa kwenda Madrid ya Wanawake.
BAADA ya kiungo mshambuliaji Hasnath Ubamba kuuzwa na FC Masar kwenda Madrid CFF ya Hispania, inaelezwa kuwa Fountain Gate Princess itanufaika kwa kupata asilimia 20 ya ada ya uhamisho huo kutokana na makubaliano yaliyowekwa kwenye mkataba wakati awali anatua Misri.
Ubamba aliitumikia FC Masar inayoshiriki Ligi Kuu Soka Wanawake Misri kwa misimu miwili baada ya kuuzwa na Fountain Gate Princess mwaka 2024 kwa mkataba wa miaka mitatu ambapo umebaki mwaka mmoja ndipo akauzwa kwenda Madrid ya Wanawake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Rais wa Fountain Gate FC, Japhet Mboto Makau, amesema asilimia hiyo 20 ni makubaliano ya moja kwa moja kati ya FC Masar na Fountain Gate Princess.
“Hayo ni makubaliano baina ya FC Masar na Fountain kwenye mkataba wa awali wakati anaenda Misri tulikubaliana sisi tunapata asilimia 20 ya mauzo ya mchezaji,” amesema Makau na kuongeza.
“Tunafurahi kuwa moja ya timu ama akademi zinazozalisha wachezaji wengi wanaopata nafasi ligi mbalimbali, lengo ni kuwasaidia na kuwahamasisha vijana wenye vipaji.”
Uhamisho wa Ubamba kwenda Ligi Kuu ya Wanawake Hispania unafanya Tanzania kuwa na jumla ya nyota wawili wanaokipiga kwenye ligi hiyo baada ya Opah Clement kuchezea Eibar.
Ndani ya misimu miwili aliyoitumikia FC Masar, Ubamba alicheza mechi 62, akifunga mabao 30 na kutoa asisti 19.
Mafanikio makubwa kwa nyota huyo ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Misri katika misimu miwili mfululizo.
Ubingwa huo uliiwezesha FC Masar kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, ambapo msimu wa 2024/25 ilimaliza katika nafasi ya tatu, huku msimu uliofuata ikishika nafasi ya nne. Katika mashindano hayo, Ubamba alicheza dakika zote na kutwaa tuzo moja ya mchezaji bora wa mechi.