Fountain Gate haoo kileleni wakiinyoosha Ken Gold

Fountain Gate wakipongezana baada ya ushindi dhidi ya Ken Gold
Mbeya. Fountain Gate imeendelea kutesa kwenye Championship baada ya leo kuibamiza Ken Gold bao 1-0 na kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi hiyo kusaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
Ushindi huo unakuwa wa nne mfululizo kwa timu hiyo ya jijini Dodoma na kufikisha pointi 12 na sasa inasubiri matokeo ya kesho ya Mbuni wenye alama tisa na mabao 10 ya kufunga na kuamua atakayesimama rasmi kileleni baada ya michezo minne.
Katka mchezo wa leo Jumapili uliopigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa Ken Gold walianza kwa kasi na presha kubwa ya kupata mabao ya haraka, lakini wapinzani walikuwa imara kutibua mipango kwa kuondosha hatari zote.
Pamoja na kwenda mapumziko kwa nguvu sawa ya bila kufungana, lakini wenyeji walishindwa wao kutokana na kukosa bao dakika ya 14 baada ya Elisha Anthony mpira wake wa penalti kugonga nguzo na kurudi uwanjani kabla ya kuupiga tena na kutoka nje.
Fountain Gate nao waliitengeneza nafasi tatu ikiwamo kona moja ambazo pengine zingewanufaisha lakini mipira yao haikuwa na macho kuliona lango la wapinzani.
Kipindi cha pili kwa Fountain Gate wakiwatoa Mussa Majuto, Salum Chubi na Daniel Joram na kuingia Said Bakari, Salim Aiyee na Ibrahim Mgecha, huku Ken Gold iliwapumzisha Renatus Mafuru, Moshi Mrisho na kuingiza Kigy Makasi na Fred Zeno dakika ya 59 na 66.
Mabadiliko yaliipa faida Fountain Gate waliopata bao dakika ya 82 kupitia kwa Bakari aliyetokea benchi akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Mgecha na kuongeza morali kwa timu hiyo na kuutawala mchezo dhidi ya wenyeji walioonekana kuelemewa na kochoka.
Timu hiyo ambayo ni msimu wa tatu kucheza michuano hiyo, walionesha soka safi wakicheza kwa umakini na utulivu dhidi ya wapinzani waliokuwa uwanja wa nyumbani na kufanikiwa kuondoka na alama tatu na sasa wanajiandaa na mchezo ujao na JKT Tanzania ugenini.