Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fomesheni za ajabu Sauzi

Carlos Parreir

Frank Sanga, Johannesburg TATIZO la Jose Mourinho ni kutaka timu zake kuziba njia zote na kushambulia kwa machale, lakini kuna makocha wengine wameongeza uhondo kwenye fomesheni yake hiyo. Jambo kubwa ambalo limetokea katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, si Uswisi kuifunga Hispania. Huo unaweza kuwa ni miongoni mwa miujiza, lakini jambo kubwa ni kutokea kwa mapinduzi ya soka na kubadilika kwa fomesheni za uchezaji uwanjani ambazo zimeletwa na baadhi ya makocha tena wa timu ambazo hazipewi nafasi kubwa ya kufika mbali. Timu ambazo zilidhaniwa kuwa ni ndogo na kwamba hazingefika mbali, makocha wake wameonekana kuwa na mbinu nzuri zaidi na mpya kuliko makocha wanaofundisha timu kubwa. Si kwamba makocha hao wamekuja na mtindo wa kupaki gari nyuma na kushambulia kwa machale kama Mourinho anavyofanya,wao wamekuja na mbinu mpya zaidi na nzuri. Ni mbinu nzuri kwa sababu wanawaruhusu wachezaji wao kucheza mpira dakika zote tisini na si kusubiri tu nyuma kama anavyofanya Mourinho na timu zake zote. Miongoni mwa makocha wanaosifika kwa mbinu ni kocha wa Mexico, Javier Aguirre ambaye anatumia fomesheni ya 4-3-3. Hata hivyo fomesheni hiyo imekuwa ni kwenye maandishi tu, lakini si Mexico wanavyocheza uwanjani na hasa katika mechi mbili ambazo wamecheza dhidi ya wenyeji Afrika Kusini na Ufaransa katika mechi za Kundi A. Mexico ni miongoni mwa timu chache ambazo zinacheza mchezo katika fomesheni ambazo unaweza usizikute sehemu yoyote katika ulimwengu wa soka. Wanaposhambulia wanakuwa na wachezaji sita mbele huku mabeki wanne wakiwa wamesogea katika nafasi ya kiungo na wanapopokwa mpira, wachezaji sita wanarudi nyuma haraka na katikati wanabaki watatu na mmoja mbele. Ni vigumu kuelezea fomesheni ambayo Mexico wanacheza kwani si kwamba wanajihami ila wanacheza mpira kwa nidhamu ya hali ya juu na kufuata maelekezo ya kocha. Kocha msaidizi wa Bafana Bafana,Pitso Mosimane anasema hawezi kuelezea jinsi Mexico wanavyocheza ila ni timu tishio. "Hii ni timu hatari na itafanya maajabu katika fainali hizi mwaka huu, wanashambulia sita na wanazuia wakiwa sita, hii timu inatisha na wachezaji wake wana nidhamu ya hali ya juu," anasema. Mexico ambayo ilitoka sare ya bao 1-1 na Bafana Bafana katika mechi ya ufunguzi kwenye Uwanja wa Soccer City ilifanya maajabu kwa kuichakaza Ufaransa mabao 2-0 katika mechi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Peter Mokaba, mjini Polokwane. Si Mexico tu, kuna timu kama Slovenia ambayo imewashangaza watu wengi kwa kucheza kandanda safi na kuvutia huku nao wakicheza kwa fomesheni ya kimaandishi: 4-3-3. Lakini uwanjani kikosi hicho cha Matjaz Kek kimekuwa kikicheza tofauti kabisa; wanapenda kucheza muda mwingi upande wao huku wakienda mbele taratibu kwa mfumo wa wachezaji watatu kwenda kwa mtindo wa pembe tatu mpaka wanapofika mahali na kuwaacha wengine kuendelea hivyo. Ni timu ambayo mabeki wake wanne hawaondoki nyuma hata kama wanashambulia na wanaposhambuliwa kunakuwa na wachezaji wengine wawili wanarudi kuwasaidia na kufanya wawe sita, kiungo wanabaki watatu na mshambuliaji mmoja. "Mpira wa sasa ni kocha mwenyewe kuamua unataka timu yako icheze vipi, hakuna tena mambo ya fomesheni, angalia mpinzani wako anavyocheza na weka mbinu zako. Ona jinsi Slovenia wanavyowachezea Marekani," anasema mwandishi wa michezo wa Shirikia la Habari la Senegal (APS), Selif Diallo wakati akiangalia mechi hiyo akiwa na mwandishi wa makala haya kwenye Uwanja wa Ellis Park. "Haya mambo ya kutaka kucheza samba tuyaache kwa Brazil, mambo ya fomesheni za 4-4-2 au 4-3-3, nadhani sasa yamepitwa na wakati, ukiangalia fainali hizi unajua kuwa kuna mapinduzi makubwa yanakuja, kila kocha ana fomesheni yake," anasema. Uchezaji wa timu zinazoonekana ndogo katika fainali hizo,umekuwa ukivutia mashabiki wengi na wanasema kumbe inawezekana kwa kila kocha kuwa na fomesheni yake ikafanya kazi. Algeria ilipocheza na England ilifanya hivyo kwa kuwa na mabeki wanne nyuma ambao walikuwa hawaondoki kabisa hata wanaposhambulia na waliposhambuliwa waliongezeka wawili zaidi wakiaacha viungo wawili na mshambuliaji mmoja. "Huu ndio mpira ambao tunataka kuona, acha timu kubwa zije na fomesheni zao ambazo zimezoeleka, mpira wa kisasa ni kila kocha kuwa na fomesheni yake, kama kuna makocha 200 duniani wanaofundisha timu za taifa, tunataka tuone pia kukiwa na fomesheni 200, na ukiangalia fainali hizi huko ndiko tunakokwenda," anasema Diallo. Timu nyingine ambazo zimevutia kwa kucheza kwa pamoja na kushambulia zikiwa na wachezaji wengi mbele na kuzuia zikiwa pia na wachezaji wengi nyuma ni Korea Kaskakazini na Uswisi. Brazil licha ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Korea Kaskazini ilibidi itumie nguvu na maarifa ya hali ya juu mpaka kipindi cha pili ilipopata mabao hayo. Uswisi licha ya kushambuliwa na Hispania walicheza kwa mbinu zaidi na ufundi huku wakijituma na kucheza kwa melengo dhidi ya timu hiyo inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa dunia na hata wakashinda 1-0. Je haya yanaweza kuwa mapinduzi ya soka na kuanzishwa kwa fomesheni mpya katika soka,ni suala ambalo linahitaji mjadala zaidi.