Flora mjengo aliounyesha H.Baba ni wetu

Muktasari:
- Nyumba hiyo, H. Baba ameamua kuiita Big Brother Mwanza, aliionyesha kwa mara ya kwanza Machi 23 mwaka huu mtandaoni na kuzuagumzo huku wengine wakisema kafanya vile kwa ajili ya kuuza sura kwa kuwa ni dalali wa nyumba.
Dar es Salaam. Siku chache baada ya msanii wa Bongo Fleva, Hamisi Ramadhani ’H.Baba’ kuonyesha nyumba yake wa ghorofa uliopo Jijini Mwanza na watu kudai siyo wake, mkewe Flora Mvungi, amekanusha uvumi huo.
Nyumba hiyo, H. Baba ameamua kuiita Big Brother Mwanza, aliionyesha kwa mara ya kwanza Machi 23 mwaka huu mtandaoni na kuzuagumzo huku wengine wakisema kafanya vile kwa ajili ya kuuza sura kwa kuwa ni dalali wa nyumba.
Akizungumza na MCL Digital, Flora alisema nyumba hiyo ni yao na hawajaanza kuijenga leo, kwani iliwachukua zaidi ya miaka mitatu hadi kuifikia hapo ilipo na kuwataka watu waache kubeza mafaniko hayo.
“Nimesikia kwenye mitando watu wakiponda kuwa nyumba hiyo siyo ya H. Baba mara anaifanyia udalali, wakati sio kweli naomba waamini kwamba ni ya kwetu na kupuuza maneno yanayosemwa na watu kwa malengo wanayoyajua wao japo hilo nililijua tangu mwanzo, lakini ndio hivyo huwezi kuwazuia binadamu kusema,” alisema Flora.
Alipoulizwa kama anaona kuna faida yoyote ya kuonyesha nyumba hiyo, Flora alisema kwa upande mwingine anaona sawa kwa kuwa mashabiki wa H. Baba pia wangependa kujua maendeleo ambayo kayafikia ukizingatia kwamba wasanii wamekuwa wakidharaulika kuwa hawana maendeleo.
Kuhusu hatma yake katika tasnia ya filamu, Flora alisema alikuwa analea mtoto wake kwa sasa amefikisha miaka mitatu hivyo alisimama kidogo kwenye kazi kwa ajili ya ulezi.
Vilevile kwa sasa ameamua kurudi darasani kwa kujiendeleza kusomea fani ya uandishi wa habari, baada ya kuikacha miaka tisa iliyopita.
Flora ambaye aliwahi kutesa na kipindi cha Bongo Dar es Salaam, alisema suala la kusafiri mara kwa mara wakati kundi lao likiwa moto ndilo lilolasababisha kuacha kuendelea na masomo yake.
Hata hivyo, anakiri huenda utoto ulikuwa unamsumbua, lakini sasa hivi baada ya kukaa na kutafakari ameona kuna haja ya kurudi darasani.
“Nadhani wakati ule utoto ulikuwa mwingi, sikujua nini sahihi cha kuchagua, lakini kwa kuwa nishayaona maisha na nishatambua mimi ni nani nimeamua kurudi darasani huku matarajio yangu yakiwa ni kuwa Ofisa Uhusiano wa moja ya makampuni, shirika au taasisi,”alisema Flora.