Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

First Eleven Yanga inayotesa Uturuki

Kikosi cha Yanga kinachoshiriki mechi za kirafiki Uturuki

KAMBI ya Yanga inayoingia siku ya tisa leo Jumanne mjini hapa imeanza kuonyesha mabadiliko chanya kikosini katika mambo mawili. Mosi, kujiamini kumeongezeka na pili staili ya uchezaji imebadilika na kuwa ya pasi ndefu tofauti na jambo lililokwenda pamoja na mabadiliko ya kikosi cha kwanza. Kocha Ernest Brandts, ambaye hakuwa na kikosi cha kwanza maalumu wakati anaanza kazi, alisitisha likizo yake baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara akiomba wiki tatu za mazoezi ya nguvu ikiwamo wiki mbili za kambi hapa Uturuki. Tayari Yanga inayoendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Fame unaomilikiwa na hoteli iliyofikia ya Fame Residence hapa Antalya, imecheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Arminia Bielefeld na kutoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Adora uliopo kilomita zaidi ya 20 kutoka kambini. Wachezaji wa Yanga ambao hufanya mazoezi makali kwa saa mbili kila asubuhi na jioni, wameonekana kuwa na ari ya hali ya juu na wanajiamini zaidi katika uchezaji tofauti na ilivyokuwa awali ambapo wengi wao walikuwa hawajazoea staili na mifumo ya Brandts. Mazoezi ya utulivu kwenye uwanja wa kisasa yamebadili wachezaji hao ambao kiungo mmoja alisikika akisema: 'Kama siku zote tungekuwa hapa mbona tungekuwa mbali sana.' Ushindani wa namba umezidi kuongezeka hususan kwenye ulinzi na kiungo kutokana na kila mmoja kutaka kumshawishi kocha kwamba ana kitu cha kipekee na katika kila kipindi cha mazoezi kocha amekuwa akijaribu kitu kipya kuona nani anaweza nini kwenye nafasi gani na tayari picha ya kikosi kipya cha kwanza imeshaonekana mazoezini. Tofauti na awali wakati walipokuwa wanapiga pasi nyingi fupi, sasa wanasisitizwa kupiga pasi ndefu kwa kasi na kubadilishana nafasi haraka ili kuchanganya mpinzani jambo ambalo wameonyesha kuliweza ingawa bado kwenye umaliziaji kuna tatizo. Mastraika wamekuwa wakipewa msisitizo waongeze umakini zaidi kwa kutumia nafasi zinazotengenezwa na viungo ambao nao pia wamebadilishwa. Katika mechi dhidi ya Arminia timu hiyo ilianza kuonyesha mabadiliko kwa kucheza pasi hizo ingawa ilikosa mabao mengi huku kocha akiwasisitizia wachezaji kucheza zaidi kwa kufungua uwanja na pasi zao ndefu kwa kuwatumia zaidi Haruna Niyonzima 'Fabregas' na David Luhende ambao anataka kuwaimarisha wasimame pembeni kwenye winga ingawa na kiraka Nurdin Bakari naye anaiweza nafasi hiyo. Kwa staili ya mazoezi na hali iliyojionyesha kwenye mechi ya kwanza ya kirafiki kikosi kipya cha kwanza huenda kikawa hivi: Ally Mustapha 'Barthez', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athuman Idd 'Chuji'/Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Kabange Twite, Said Bahanuzi, Didier Kavumbagu, Nurdin Bakari/David Luhende. Hakuna ubishi kwamba Barthez yuko fiti kwa sasa na ndiye atakayeanza langoni huku kwenye ulinzi Yondani na Cannavaro wakibaki kusimama katikati kutokana na kujiamini kwao na kutokuwa na makosa mengi, kushoto Joshua ana nafasi kubwa ingawa Stephano Mwasika alikuwa bado hajapewa nafasi. Kuna kila dalili Mwasika atasogezwa namba za mbele pembeni na kwenye kiungo. Beki wa kulia atasimama Mbuyu Twite. Katika kiungo Chuji na Frank Domayo wanachuana vikali na mmoja wao atacheza na Kabange Twite ambaye amefiti kwenye namba nane na mchezo unavyobadilika unaweza kudhani ni straika kwani namba zote za mbele anacheza vizuri. Niyonzima anamchezesha kama winga wa kulia na kushoto anamchezesha Luhende ingawa na Nurdin naye ameonekana kuimudu kama ilivyo kuwa Simon Msuva. Kwenye ushambuliaji Bahanuzi na Kavumbagu ndio wanaonekana kupendelewa zaidi ingawa Tegete naye yupo fiti kama alivyoingia na kupachika bao kwenye mechi ya Jumamosi iliyopita dhidi ya Arminia. Katika kikosi hicho cha kwanza wachezaji ambao hadi sasa wanaonekana kuwa na nafasi kubwa ya namba za kudumu ni Mbuyu Twite na Kabange Twite ambao ni viraka wenye uwezo wa kucheza namba nyingi uwanjani, Yondani na Cannavaro, Joshua, Barthez, Kavumbagu na Niyonzima ambaye anachezeshwa pembeni lakini mara nyingi hujisahau na kujikuta akirudi katikati. Kocha wa Arminia Bielefeld aliiambia Mwanaspoti hivi: "Hii timu ina wachezaji wenye kasi na imenipa changamoto sana na wachezaji wake wanabadilika sana. Unatakiwa kuwa na wachezaji wanaotumia akili za haraka na wenye kasi ili kukabiliana nao viungo wao wana nguvu sana na wanajaaa katikati," alisema kocha huyo ambaye kwenye kikosi chake ana Waghana wawili; beki na straika. "Wanacheza mpira fulani wa kuonana sikutarajia kama wangecheza soka ya juu kiasi hiki, mimi nilidhani ni mazoezi tu laini laini ila imetoa changamoto sana kwa timu yangu wanashambulia vizuri na wana pasi nzuri, ila wanahitaji kuwa makini kwenye umaliziaji, wana mastraika warefu wazuri ambao bado wanahitaji kujituma zaidi. "Lakini wamenipa mazoezi mazuri sana, natamani ningecheza nao tena. Inaonekana wana mazoezi ya muda mrefu sana kwa vile wanacheza kitimu, ni mpira mzuri wa staili ya Kiafrika, nimependa sana,"alisisitiza kocha huyo kijana ambaye atakuwa mjini hapa kwa wiki tatu kuiandaa timu yake kwa Ligi Daraja la Tatu Ujerumani. Timu hiyo ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu Ujerumani mwaka 2009.