Feisal aaga rasmi, Yanga yaweka ngumu

Muktasari:

  • Kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameaga rasmi Yanga baada ya kuwepo na tetesi kuwa amesaini na timu ya Azam FC.

NYOTA wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto' amewaaga rasmi mashabiki wa timu hiyo huku ikielezwa anajiunga na Azam FC.

Kupitia barua iliyochapishwa na nyota huyo kupitia mtandao yake ya kijamii aliandika "Umekuwa wakati mzuri sana wa kuichezea Klabu ya Yanga yenye historia kubwa na ya kuvutia nchini na Afrika yote,"

"Tumekuwa na nyakati nyingi mchanganyiko, tulifurahi pamoja pale furaha ilipokuja uelekeo wetu na tulihuzunika pamoja nyakati mbaya zilipotutokea, nitakumbuka mengi mazuri yaliyotokea pamoja na nitasahau yote mabaya kwa haraka sana,"

"Kila nikiwakumbuka mashabiki wa Wananchi moyo unakuwa mzito kuwaaga hivyo hivyo kwa wachezaji wenzangu na viongozi pia kwa upendo mlionionyesha tukiwa pamoja kwenye shida na raha lakini lisilo budi hutendwa au hunenwa kwa hiyo leo nasema Kwaherini Wananchi,"

"Ila maisha ndivyo yalivyo mambo huja na kupita na kuna wakati yanajirudia, mpaka wakati mwingine tena, kwa heri ya kuonana," ilisomeka taarifa hiyo.

Wakati Feisal akiaga taarifa iliyotolewa na Klabu hiyo iliendelea kusisitiza kwamba nyota huyo bado ni mali yao kwani ana mkataba hadi kufikia Mei 30, 2024 na tayari walianza mazungumzo na wawakilishi wake wakiongozwa na Mama yake mzazi ili kuboresha maslahi yake.

Taarifa hiyo iliendelea kwa kueleza kwamba haijapokea majibu mbadala ya mapendekezo ya maboresho hayo kutoka upande wa Feisal na wawakilishi wake na badala yake walipokea barua ya kuvunja makataba wake ambao ni kinyume na makubaliano.

Aidha Yanga ilisema kwamba imesharejesha kiasi cha Sh112, 000, 000 milioni ambazo Feisal aliziweka katika Akaunti ya Klabu hivyo kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na FIFA ni lazima zifuatwe na timu yoyote inayotaka kumsajili mchezaji wa Yanga.