Fei Toto aanika uchawi!

Saturday June 19 2021
fei pic
By Olipa Assa

KIUNGO fundi wa mpira, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amefichua kitu kinachombeba na kuwa moto kwenye Ligi Kuu Bara, akidai uzoefu alioupata na kujibidiisha kwake ndiko kulikomfikisha alipo.

Fei alisajiliwa na Yanga 2018 akitokea JKU ya Zanzibar na amekuwa mmoja ya wachezaji tegemeo kwa sasa tofauti na ilivyokuwa awali naye alisema kudumu kwake Jangwani na kuaminiwa ndiko kulikomfanya aingize vitu vingi kichwani mwake, vitakavyomsaidia kukifisha mbali kipaji chake.

“Nilivyoingia Yanga kwa mara ya kwanza ni tofauti na nilivyo sasa, nimeongeza maarifa mapya na naendelea kujifunza kwa kadri ninavyoweza ili kuendelea kukiboresha kipaji changu kusonga mbele na sio kurudi nyuma,” alisema Fei na kuongeza;

“Akili yangu imekomaa na sio mwisho kwani soka linahitaji mafunzo kila siku, sitaacha kujifunza kwani lengo langu ni kuhakikisha nafika mbali kwa maana ya kucheza nje, hilo linawezekana na lipo ndani ya uwezo wangu.”

Kiungo huyo mwenye bao moja hadi sasa katika Ligi Kuu, alikiri msimu huu kumekuwa na ushindani katika ligi hiyo na hilo linamfanya asibweteke kupambania namba kikosi cha kwanza bila kujali anaanzishwa na makocha tofauti waliopo na waliopita ndani ya kikosi hicho.

“Ujue wengi wananidhania ninajibweteka kwa vile naanza kikosi cha kwanza, siwezi kufanya hivyo naendelea kujituma na kupamba kadri niwezavyo ili kuendelea kuboresha kipaji changu,” alisema.

Advertisement
Advertisement