Farid apania kurudi kibabe

Muktasari:

NYOTA wa Yanga SC, Farid Mussa ambaye alikuwa akisumbuliwa na majeraha kwa wiki kadhaa kabla ya kuugua Malaria, amewatuliza Wananchi kwa kusema bado anahisi kuwa anadeni nao na amepanga kuonyesha makali yake kwenye michezo mitano iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara ‘TPL’.

NYOTA wa Yanga SC, Farid Mussa ambaye alikuwa akisumbuliwa na majeraha kwa wiki kadhaa kabla ya kuugua Malaria, amewatuliza Wananchi kwa kusema bado anahisi kuwa anadeni nao na amepanga kuonyesha makali yake kwenye michezo mitano iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara ‘TPL’.

Agosti mwaka jana, Farid ajiunga na Yanga akitokea Hispania ambako alikuwa akikichezea kikosi B cha CD Tenerife, kwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja ambao unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Farid alisema kwa kiasi fulani majeraha yalimrudisha nyuma lakini anaamini anaweza kufanya vizuri kwenye michezo mitano iliyosaliwa kwa Yanga ambayo ni dhidi ya Ruvu Shooting, Mwadui, Simba, Ihefu na Dodoma Jiji.

“Bado kuna michezo mbele, nimekuwa nikipambana mazoezini ili kurudi nikiwa bora zaidi kwa sababu kuna kipindi nilikuwa majerahi na nilivyopona nikaumwa tena, naamini mambo yatakuwa mazuri na bado nafasi ipo kwenye ya kumaliza vizuri msimu,”

“Hatuwezi kukataa na kuona kana kwamba ligi ndio imeisha lolote laweza kutokea huu ni mpira,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Azam.

Farid aliongeza kwa sasa anacholenga ni kulipa deni kwa mashabiki wa Yanga kwenye michezo iliyobaki kuhusu kuongeza mkataba au laa ni mara baada ya kumalizika kwa msimu, Juni kwani akili yake kwa sasa ipo kwenye mechi zao zilizosalia.

Baada ya kuachana na CD Tenerife, Farid alikuwa na mipango ya kuendelea kucheza soka la kulipwa barani Ulaya lakini kuchachamaa kwa janga la virusi vya corona ndio kitu ambacho kilichochea kufanya uamuzi ya kujiunga na Yanga. Yanga inapambana kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara.