Faida, athari Panga pangua Yanga

Wakati Yanga ikifanya usajili wa wachezaji wapya tisa mpaka jana, huku ikiwaacha kadhaa, usajili huo umewaibua baadhi ya makocha nchini ambao wameeleza faida na hasara za panga pangua.

Yanga imewasajili makipa Diarra Djigui na Erick Johora; mabeki Djuma Shaban na David Bryson; mawinga Dickson Ambundo, Yusuph Athuman, Khalid Aucho na washambuliaji Heritier Makambo na Fiston Mayele.

Msimu uliopita Yanga iliwasajili Farouk Shikhalo, Lamine Moro, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Haruna Niyonzima, Carlos Carlinhos, Michael Sarpong, Sogne Yacouba, Abdulrazak Fiston na Said Ntibazonkiza, lakini waliobaki kikosini ni Yacouba na Mukoko pekee, huku Tuisila akiuzwa Morocco.

Msimu wa 2019/2020 iliwasajili David Molinga, Issa Bigilimana, Patrick Sibomana, Ulikhob Sydney, Maybin Kalengo, Juma Balinya, Pappy Tshishimbi, Bernard Morrison, Yassin Mustafa, Erick Tshishimbi, Lamine na Shikhalo, lakini iliachana wengi na kubaki na Lamine na Shikhalo ambao pia msimu huu imeachana nao.

Panga pangua hiyo imewaibua makocha walioeleza faida na athari za ingizo jipya kwenye kikosi hicho kinachojiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika baadaye.

Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza alisema changamoto itakuwa ni wachezaji iliowaleta Yanga Tanzania soka kuwakubali au vinginevyo.

“Ni kweli kuongeza na kupunguza idadi kubwa ya wachezaji kwa pamoja huwa kuna changamoto zake, lakini ubora na aina ya wachezaji ambao Yanga imekwishawasajili kipindi hiki kwangu ni usajili bora tangu nimeanza kuifahamu timu hiyo,” alisema.

“Tangu niifahamu Yanga hii ni mara ya kwanza inafanya usajili mzuri mno, Aucho ni kiungo wa kati bora zaidi kwangu, akicheza na Mukoko kutakuwa na kombinesheni kali.”

Kocha Abdallah Kibadeni alisema kwa usajili ilioufanya Yanga inaonekana bado wako katika mchakato wa kujenga timu.

“Timu kupata muunganiko sio kazi nyepesi, ingawa kwa ubora wa wachezaji iliowasajili hata kama timu haitakuwa katika kiwago bora, lakini wachezaji mmojammoja wanatoa uhakika wa kuisaidia,” alisema.

Aliyewahi kuwa kocha wa makipa wa timu hiyo, Juma Pondamali alisema usajili huo unaonyesha kuchuja pumba na mchele.

“Wanajitahidi sana, tofauti na misimu miwili iliyopita mfano kipa wa Mali ana sifa nne ambazo zinasababisha nimkubali,” alisema Pondamali, kipa wa zamani wa Yanga na Stars.

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema kwenye usajili inaonekana benchi la ufundi la Yanga bado linaendelea kujijenga.

“Bahati mbaya hakuna pre-season (maandalizi), labda hizo wiki mbili wanazokwenda Morocco, mechi za kirafiki kule zitawasaidia,” alisema Mayay.