Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Eeh! Kumbe kikapu ndo hivi!

Hasheem Thabit.

Muktasari:

Watu wa rika mbalimbali wamekuwa wakifuatilia soka, mpira wa kikapu, kriketi, magongo, ngumi, netiboli, wavu, ragbi, kuogelea, gofu pamoja na tenisi.

        KATIKA dunia tunaoishi ipo michezo mingi ambayo kama ukianza kuihesabu itakutafunia muda wako kwani ni mingi, ingawa ipo michezo kama 10 ambayo ndiyo maarufu zaidi na imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na mashabiki wengi.

Watu wa rika mbalimbali wamekuwa wakifuatilia soka, mpira wa kikapu, kriketi, magongo, ngumi, netiboli, wavu, ragbi, kuogelea, gofu pamoja na tenisi.

Hata hivyo, kama haujui ni kwamba dunia nzima mchezo unaoongozwa kwa kupenda na kukusanyaa mashabiki engi ni soka ikisadikiwa kuwa zaidi ya mashabiki kuanzia 3.3 hadi 3.5 bilioni wanaushabikia mchezo huo, ukifuatiwa kwa karibu na mpira wa kikapu wenye mashabiki kuanzia 2-3 bilioni kwa mujibu wa mitandao mbalimbali ikiwemo mtandao wa Total Sportek na Fobres.

Soka linatajwa kama mchezo unaongoza dunia nzima na wachezaji wa mchezo huo wamekuwa matajiri kupita kiasi kutokana na miguu yao inavyofanyakazi lakini unatajwa kama mchezo wa walalahoi ukilinganisha na kikapu ambao kwa asili tu unachezwa na wachezaji waliotoka kwenye familia bora na wengi wao wameenda shule na wana kazi zao ofisini.

MVUTO

Mchezo wa kikapu una mvuto mkubwa na wenye mashabiki wengi vijana na unatajwa ndiyo unaofuatia kwa kupendwa duniani ukichezwa zaidi katika nchi za Marekani ukiwa ndiyo unaoongoza ukifuatiwa na soka. Nchi nyingine ambazo ni manazi wa mchezo huo ni Canada, China, Uturuki, Ufilipino na mataifa mengine makubwa yakiwamo ya Afrika.

Nchini Marekani mchezo wa kikapu una ligi yao maarufu kama NBA (National Basketball Association), ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na soka pia wanamichezo wanaocheza mchezo huo wametajwa kuwa ni matajiri na wenye maisha bora.

USHAHIDI

Kwa mujibu wa mtandao wa Forbes ulitoa orodha ya timu tajiri duniani katika michezo yota na kikapu umetoa timu kumi tajiri za Marekani ambazo ni Los Angeles Lakers (Dola 2.6 bilioni), New York Knicks (Dola 2.5 bilioni), Chicago Bulls (Dola 2 bilioni), Boston Celtics (Dola 1.7 bilioni), Los Angeles Clippers (Dola 1.6 bilioni), Brooklyn Nets (Dola 1.5 bilion), Golden State Warriors (Dola 1.3 bilioni), Houston Rockets (Dola 1.25 bilioni), Miam Heats (Dola 1.18 bilioni) na Dallas Maverick (Dola 1.15 bilioni).

Hata hivyo, kwa mujibu wa mtandao huo pia ulitoa wachezaji wanaoongoza kwa kupata kipato kikubwa ambao baadhi yao ni Kobe Bryant anayechezea LA Lakers, LeBron James wa Cleveland Cavaliers, Kevin Garnett wa Brooklyn Nets, mchezaji huyu aliwahi kuwa Mchezaji Bora wa NBA na aliwahi kutwaa medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Olimpiki mwaka 2000.

TANZANIA

Kwa hapa Tanzania mchezo wa kikapu haujawatoa wanamichezo wengi ukiachana na Hasheem Thabeet ambaye aliwahi kubahatika kucheza hata NBA akiwa kwenye timu ya Merphis. Hata hivyo, mchezo huu ambao umechezwa na viongozi wengi wa juu kama Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Spika mstaafu wa bunge la Jamhuri ya Tanzania, Samuel Sitta, Jaji Mstaafu, Agustino Ramadhani na wengine kibao nao si haba, unahusisha sana vijana maarufu kama ‘Mabrazameni’.

Mchezo huo kwa Tanzania hauna mashabiki wengi ukilinganisha na soka lenye mashabiki lukuki ambapo hata ikichezwa mchangani bado itajikusanyia mashabiki kibao tofauti na kikapu ambao ni mara chache sana ukauona unachezea uswazi. Mwanaspoti limefanya uchunguzi ili kubania ni kwa nini mchezo wa kikapu unakosa msisimko na unaonekana ni mchezo wa kitajiri ikiwa ni pamoja na kuchezwa sehemu maalumu pekee ukilinganisha na soka.

HUU NDIYO UKWELI

Huwezi kukuta mchezo wa kikapu ukichezwa Tandika, Temeke, Manzese labda zifungwe barabara ili yawekwe magoli kwenye barabara za lami, tofauti na soka maeneo hayo ndiyo yanayotoa wachezaji wengi kwani soka linachezwa sehemu yoyote ile na ndiyo maana kikapu unachezwa sehemu maalumu na mara nyingi ni Oysterbay, Upanga, Masaki na maeneo ya vyuo vikuu nchini.

Mwanaspoti lilifanya mahojiano na viongozi, wanamichezo pamoja na walimu kutoka shule zinazofundisha michezo hapa Tanzania ambapo Kamishina wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF) ambaye pia aliwahi kuwa mchezaji na kocha, Zabron Manase, alieleza sababu zifuatazo;

ELIMU

Manase anasema kwamba soka haichagui nani anacheza na unachezwa sehemu yoyote ili mradi tu magoli yawepo, pia ni mchezo rahisi sana ukilinganisha na kikapu ambao huwezi kuucheza mchangani na mara nyingi lugha yake ni ya Kizungu (Kiingereza), hivyo ni lazima mchezaji awe na elimu ya wastani ambayo itamsaidia kuelewa jinsi ya kuucheza.

“Wachezaji wengi wanaocheza soka wanaogopa kucheza kikapu kwa sababu ni mchezo unaotumia Kiingereza sana, ni tofauti na mchezaji kikapu mwenye uwezo wa kucheza soka pia, huyo atacheza soka kiurahisi sana, hii ni kwa sababu kikapu ‘teminology’ zake nyingi ni za lugha ya Kiingereza.

“Tuliwahi kuendesha mafunzo ya michezo yote miaka ya nyuma pale Shule ya Sekondari Makongo, baada ya mafunzo hayo tulibaini kwamba wanafunzi wote wanaopenda soka ama wanaocheza soka walikuwa watoro darasani ukilinganisha na wanaocheza kikapu, walikuwa wanakaa hadi mwisho wa vipindi vya darasani ndiyo tunaenda vipindi vya uwanjani ambapo wanasoka ndiyo huwaona tena.

MASHEFA

“Ndiyo maana pia utakuta wachezaji wa kikapu kwa hapa Tanzania na kwingine ni wafanyakazi, hiyo ni kwa sababu tayari wana elimu zao na huu mchezo ni kama ridhaa tu bado hatujafikia ngazi ya kuwa profeshono, ndiyo maana pia utawakuta wanakikapu ni mahakimu, majaji, wafanyakazi wa benki na kazi nyingine nyingi tu, sababu tu walipenda kusoma tangu shuleni.

“Kwenye soka wanamichezo wengi mpira ukiisha basi hata maisha yao yanakuwa magumu, kwa sababu tu walikuwa wavivu na watoro darasani, kwa ufupi hawapendi elimu walio wengi, ndiyo maana nguvu zao nyingi wanawekeza kwenye soka na soka likiisha baadhi yao wanaokosea kutengeneza maisha yao yanakuwa mabaya sana,”

TICHA WA MAKONGO

Mwalimu wa michezo katika Shule ya Sekondari ya Makongo ambaye pia ana leseni C ya Caf, Oscar Milambo anaelezea zaidi juu ya tofauti kati ya wachezaji wanaocheza kikapu na soka ikiwa ni pamoja na uhudhuriaji wao wa masomo.

“Unajua hapa kwetu tuna sheria kali, mwanafuzni ni lazima aingie darasani kwa ajili ya masomo haya ya kawaida, baada ya kutoka darasani kwa maana ya kwamba vipindi vikimalizika ndipo tunakuwa na vile vipindi vya michezo ambapo kila mwanafunzi anakuwa na mapenzi ya mchezo aupendao huku kila msimamizi anafuatilia kivyake kwani huwa hailazimishwi.

“Pia mchezo wa kikapu ni mchezo wenye kutumia gharama kubwa na ndiyo maana hata wanaocheza ni wale wanaotoka kwenye familia ambazo angalau zina uwezo tofauti na soka ambao ni mchezo wa maskini duniani kote. Ni rahisi pia kumtoa mchezaji wa soka kwenda kucheza kikapu kuliko anayecheza kikapu kumpelekea kwenye soka.

“Kwa vile huu mchezo unahitaji gharama kubwa ni lazima mchezaji asome ili awe na kazi ya kuweza kujigharimia kwenye vifaa na mambo mengine, jambo ambalo kwenye soka halipo, ndiyo maana pia kwenye kikapu wanachukulia kama mchezo wa kujifurahisha siyo kama ajira tofauti na soka wanapambana kwani ni ajira yao.

“Kwa nchi zilizoendelea ukichana na nchi za Ulaya, tuchukulie hata Uganda, michezo shuleni ipo kwenye silabasi zao ambapo matokeo ya mitihani ya mwisho kuna alama anazopewa mchezaji kama ufaulu wake, hapa haipo ndiyo maana unawaona walio wengi ni wasomi, kama sio wasomi basi wametoka katika familia bora wale maskini ni wachache mno,” anafichua Milambo.

Unadhani kwa nini Kikapu kimeshindwa kusambaa nchini nzima kama soka? Endelea na makala haya kesho Ijumaa ujue ukweli wake.     

Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwanaspoti au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz