Edo Kumwembe ataka historia mpya Tanzania

Muktasari:
Tanzania inahitaji ushindi dhidi ya Uganda ifuzu Fainali za Mataifa Afrika, pia ikiomba dua Cape Verde ishinde nyumbani au kupata sare dhidi ya Lesotho.
Dar es Salaam. Mchambuzi na Mwandishi wa Mwanaspoti, Edo Kumwembe amesema ni wakati wa Watanzania kuunganisha nguvu kuhakikisha taifa linaingia katika historia mpya.
Kumwembe ameyasema hayo leo katika mkutano maalum wa uhamasishaji kuelekea mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Uganda.
Amesema wakati Stars inafuzu mara ya mwisho katika fainali hizo imepita miaka mingi kwa kizazi kirefu kukosa kuona tukio hilo.
Ameongeza miaka mingi Watanzania wamekuwa wakichagua timu mbalimbali za magharibi na Kaskazini mwa Afrika kuzishabikia katika fainali hizo.
Amesema sasa ni wakati wa kizazi cha sasa kuwa sehemu ya historia wakishuhudia timu ya taifa lao ilicheza fainali hizo za mwaka huu zitakazofanyika baadaye Juni nchini Misri.