Prime
Dube ndo basi tena Azam FC

HATIMAYE mshambuliaji Prince Dube ameamua kuweka wazi kila kitu kuhusiana na klabu anayoichezea ya Azam FC na kusema wazi kwamba, harudi tena ndani ya timu hiyo na kwamba kama kuna mtu ana maswali basi waliulizwe zaidi viongozi watafafanua.
Dube imedaiwa aliandika barua ya kuomba kuondoka Azam baada ya awali kufanya mgomo baridi wa kutoambatana na timu hiyo kwenye mechi za Ligi Kuu za ugenini, lakini imebainika wazi kwamba mchezaji huyo ndo basi tena Azam.
Mwanaspoti liliamua kumtafuta mchezaji huyo kutaka kujua sababu ya kufuta kila kitu kinachomtambulisha na Azam naye alijibu kwa kifupi;
"Sina wakati mzuri wa kujibu jambo hilo, wapigie viongozi wa Azam na meneja wangu watawaambia kila kitu kitu kuhusiana na hilo."
Ishu ipo hivi. Mwanaspoti jana liliripoti kuwa mchezaji huyo alikutana na Kocha Mkuu wa Azam, Youssouf Dabo kwa ajili ya kufahamu shida ilipo na kumuahidi kurudi kuendelea na kazi, lakini sakata jipya ni kwamba staa huyo hawezi kurudi.
Jambo hilo limeendelea kuwa kubwa, baada ya Dube kwenda mbali zaidi kwa kufuta picha zote kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii (Instagram) ambazo amevaa jezi za Azam na kama haitoshi katoa utambulisho wa kuwa mtumishi wa timu hiyo.
Ni kawaida ya Mwanaspoti kukutafutia exclusive kama linavyokuleta ishu nzima kutoka kwa marafiki zake wa karibu na uongozi wa Azam kupitia kwa msemaji wa timu hiyo.
Baada ya hapo habari za uhakika kutoka kwa rafiki yake wa karibu kuwa mshambuliaji huyo alimpigia tena kocha na kumuambia kuwa alimkubalia kuwa angerudi Chamazi, ili kumpa moyo tu lakini hana mpango wa kurudi tena Chamazi.
"Ni kweli alikuja kufanya mazungumzo na kocha, lakini mara baada ya kugeuza mgongo wake alipiga simu akimuambia kocha kuwa hawezi kurudi alimkubalia kwa sababu alitaka kumheshimu lakini hawezi kurudi nyuma kwa uamuzi alioamua kuuchukua."
Chanzo hicho pia kililiambia Mwanaspoti, mbali na kumrudia kocha kwa kumpa ukweli kwa njia ya simu mshambuliaji huyo amechukua uamuzi wa kukabidhi nyumba aliyopewa na timu hiyo.
Pia amefuta picha za timu hiyo pamoja na utambulisho kuwa ni mchezaji wa Azam FC kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii 'Instagram'.
"Sio ishu ya kocha tu, Dube kaamua kwani karudisha hadi nyumba aliyokuwa amepewa na Azam kwa ajili ya kuishi ameamua kulipia hoteli wakati akisubiri kukamilika kwa ombi lake la kuvunja mkataba na timu hiyo," kilisema chanzo hicho cha karibu cha mchezaji huyo na kuongeza;
"Karudisha kila kitu hakuna kitu ambacho kinaihusu timu hiyo ambacho anakimiliki uamuzi huo unaenda sambamba na kutaka kuondoka ndani ya timu hiyo aliyoitumikia tangu 2020."
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Azam, Thabit Zakaria 'Zaka Zakazi' alisema ni kweli Dube alimpigia kocha simu na kumuambia kuwa alimkubalia kocha akimuambia atarudi kuendelea na kazi yake ndani ya timu hiyo kwa lengo la kumpa moyo tu.
"Baada ya mazungumzo na kocha na kukubali kurudi kuendelea kuitumikia Azam yalikwenda vizuri, lakini Dube mara baada ya kuondoka alipiga simu na kukiri hawezi kurudi alikuwa anampa moyo tu kocha," alisema Zaka.
Alipoulizwa kuhusiana na mshambuliaji huyo kufuta picha alishtushwa na taarifa hizo huku akisema hajaona kama zimefutwa, lakini kwa ishu ya kurudisha nyumba, Zaka alisema Duber bado anaishi kwenye nyumba za Azam na suala la kupanga hotelini, hakuwa na taarifa nalo hadi mchana wa jana.
Sakata la Dube linakaribia kufanna na lile la Feisal Salum 'Fei Toto' alipokuwa Yanga na kuamua kutangaza kuvunja mkataba kisha kuilipa klabu kiasi cha Sh 112 Milioni za uvunjwaji huo wa mkataba zikiwamo mishahara ya miezi mitatu na fedha za kulipa fidia, lakini Yanga ilimgomea kabla ya Rais Samia Suluh Hassan kuingilia kati kwa kuutaka uongozi wa Yanga kumalizana na mchezaji huyo na siku chache kuuzwa Azam anakoichezea hadi sasa.
Nyota huyo wa kimataifa wa Zimbabwe, hadi sasa amecheza dakika 734 katika dakika 1710 za mechi 19 ilizocheza Azam FC msimu huu, akiifungia jumla ya mabao saba aliyofunga kwenye mechi 12 alizocheza, huku akikosa michezo saba, huku imu hiyo ikiwa nafasi ya pili (kabla yua mechi ya usiku wa jana dhidi ya Coastal Union) ikiwa na pointi 43.