Dube awataja Bocco, Kagere

Thursday October 15 2020
dube pic

STRAIKA Prince Dube usiku wa leo anatarajiwa kuendelea kuwasha moto wakati chama lake la Azam FC litakapoikaribisha Mwadui katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu, lakini jamaa ameshindwa kujizuia na kuwataja mastraika wa Simba, John Bocco na Meddie Kagere.

Kinara huyo wa mabao wa sasa katika ligi, alisema nje ya kikosi chake katika soka la Bongo anawakubali nyota hao wa Simba na kuna vitu anaiga kutoka kwao akiamini vinamsaidia kuwa mkali zaidi ndani ya ligi hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dube alisema anapokuwa anawaangalia wachezaji hao kuna vitu ambavyo anaviongeza katika uchezaji wake ili kuwa bora zaidi anapokuwa uwanjani.

“Nawapenda Bocco na Kagere, ni wachezaji wenye ubora, nawaheshimu sana na muda mwingine huwa najifunza kitu kimoja au viwili ninapokuwa nawaangalia wakiwa wanacheza,” alisema Dube mwenye mabao matano kwa sasa na kaiweka timu yake kileleni ikishinda mechi zote tano.

Dube alisema katika upande wa Ligi ya Tanzania ameikuta ikiwa ni bora na anajivunia kuwa sehemu ya wachezaji ambao wapo katika ligi ambayo ina ushindani wa kutosha.

“Ni ligi nzuri na ina ushindani, lakini pia ina watu wenye uwezo wengi, nashukuru kuwa sehemu ya wachezaji wanaocheza ligi hii,” alisema Dube, raia kutoka Zimbabwe aliyejiunga Azam FC msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili akitokea klabu ya Highlanders.

Advertisement
Advertisement