Dube atinga rasmi TFF

SAKATA la mshambuliaji mtoro wa Azam FC, Prince Dube limechukua sura mpya baada ya mchezaji huyo raia wa Zimbabwe kuukana mkataba na klabu hiyo ya Chamazi.

Taarifa za ndani kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zinasema Dube alipeleka malalamiko yake akisema mkataba wake na Azam FC utaisha mwishoni mwa msimu huu na siyo 2026 kama taarifa ya Azam FC ilivyosema awali.

Staa huyo amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa ikiwemo Al Hilal na Simba ambazo Azam wamezichomolea ofa zao. Inaelezwa kwamba watu wa karibu na Yanga wamemhifadhi mchezaji huyo jijini Dar es Salaam na wameshampa ofa ya miaka miwili, wamemnunulia thamani za ndani za Sh30 milioni na ulinzi mkali wa saa 24 ambao alikwenda nao hadi TFF.

Watu hao wa Yanga licha ya kwamba hawajaenda rasmi Azam wamemuongezea ulinzi huo kwani hawataki abughudhiwe na wapinzani wao hususan Simba ambao wanamtaka kwa udi na uvumba.   

Kwenye taarifa ya Azam waliyoitoa kuhusu Dube kuomba kuvunja mkataba, walisema mkataba wao na mchezaji huyo utaisha mwaka 2026 na Mwanaspoti limeambiwa wanamuuza Sh700 milioni wakati yeye alishawaomba awarudishie milioni 500 walizompa wakati wa kusaini mkataba ili waachane kiroho safi.

Dube alijiunga na Azam FC Agosti 2020 kwa mkataba wa miaka miwili hadi 2022. Mwaka mmoja baadaye, 2021, alisaini nyongeza ya mkataba hadi 2024.

Huo ndiyo mkataba ambao Dube anadai kuutambua. Lakini Azam FC wanadai kwamba mwaka 2023 Dube alisaini tena mkataba hadi 2026. Huu ndiyo mkataba ambao nyota huyo anaukana.

Mwanaspoti lilimtafuta wakala wa Prince Dube, Gerge Deda kutoka Zimbabwe kupata taarifa kutoka upande wao, lakini hadi tunakwenda mitamboni hakupatikana wala ujumbe wa simu aliotumiwa haukujibiwa.

Mkuu wa Idara ya Habari ya Azam FC, Zaka Zakazi, alipotakiwa kutolea ufafanuzi suala hili, alisema kama klabu hawajapata taarifa rasmi na hawawezi kujibu zisizo rasmi. Sakata la Dube linataka kufanana na kesi kadhaa za wachezaji wa ligi ya Tanzania.


BERNARD MORRISON VS YANGA 2020

Mchezaji huyo raia wa Ghana alijiunga na Yanga, Januari 2020 akisaini mkataba wa miezi sita.

Baada ya miezi michache Yanga ilitoa picha za mchezaji huyo akiwa na rais wa sasa wa timu hiyo, Hersi Said ikisema amesaini nyongeza ya mkataba.

Lakini mwisho wa msimu, Bernard Morrison alisema hakusaini nyongeza ya mkataba na hata zile picha aliombwa apige ili kutuliza upepo.

Wakati sakata likiendelea, Morrison akatambulishwa na Simba.

Kesi ikaenda TFF na Yanga waka- shindwa. Wakakata rufaa kwenye mahakama ya michezo, Fifa ambako pia walishindwa na Morrison akajiunga na Simba kwa ajili ya msimu wa 2020/21.


RAMADHAN SINGANO VS SIMBA 2025

Mwaka 2015 chipukizi wa Simba kutoka timu ya vijana, Ramadhan Singano alikana mkataba wake na klabu hiyo akisema haukuwa mrefu kama Simba ilivyodai.

Singano alisema mkataba wake na klabu hiyo ulikuwa wa miaka miwili na ndiyo ulikuwa unaisha baada ya msimu wa 2014/15.

Lakini, Simba ilisema alisaini miaka mitatu na mkataba ulitakiwa kuisha baada ya msimu wa 2015/16.

Kesi ikaenda TFF na kupigwa sarakasi, ambapo ile ya msingi ılıtupwa na kuibuliwa kesi mpya ya Simba kutotimiza vipengele vya mkataba ikiwemo bima ya afya na makazi.

Hata hivyo, Simba ilidai ilikuwa ikimpa pesa hizo mchezaji huyo kwenye jumuisho la pamoja la mshahara wake, lakini  alikana hilo na akataka Simba ithibitishe kwa stakabadhi za malipo.

Timu hiyo ilisema uangaliwe mshahara wa mchezaji huyo kwenye mkataba na iangaliwe pesa aliyokuwa akilipwa kama mshahara.

Ukweli ilionekana alikuwa akilipwa pesa nyingi kuliko mshahara wake, lakini hilo ongezeko halikuwa na maelezo ya maandishi.

Simba ilidai ongezeko ndiyo fedha za makazi na bima ya afya, lakini ilisema kwa mdomo tu na kamati ikatupilia mbali kesi na kumtangaza Singano kuwa mchezaji huru akajiunga na Azam FC.


ATHUMAN IDD                 CHUJI VS SIMBA 2007

Hii ni moja ya kesi ambazo hazikuwahi kupata majibu hadi leo. Chuji alikuwa mchezaji wa Simba tangu 2005 akitokea Polisi Dodoma.

Mwaka 2007 akasema mkataba wake na Simba ulikwisha na akasaini Yanga. Simba ikadai mkataba haukuisha hivyo kesi ikaenda TFF.

Simba ilitoa mkataba wake na Chuji akatoka mkataba wake. Chuji akaikana sahihi iliyokuwa kwenye mkataba ilioutoa Simba.

Ikabidi mikataba yote ipelekwe kitengo maalumu cha  kutambua sahihi za watu na majibu hayakuwahi kutoka hadi TFF ilipoamua kuuvunja mkataba na kumuacha mchezaji huyo huru akajiunga na Yanga. Sasa ni zamu ya Prince Dube nini kitatokea? Tusubiri tuone.