Droo ya Afcon U-20 kupangwa Jumatatu

DROO ya makundi ya fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 inatarajiwa kuchezeshwa Jumatatu Januari 25 kwenye hoteli ya Hilton mjini Yaounde Cameroon kuanzia saa 5:00 asubuhi.

Timu za taifa za vijana (U-20) kutoka nchi 12 zilizofuzu kucheza michuano hiyo ambazo ni Mauritania, Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya kati, Gambia, Ghana, Morocco, Mozambique, Namibia, Tanzania, Tunisia na Uganda zinatarajiwa kushiriki katika droo hiyo ambayo huenda ikatoa makundi matatu au manne.

Timu ya taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 maarufu kama Ngorongoro Heroes ilifuzu kucheza michuano hiyo mikubwa barani Afrika baada ya kuweza kufika fainali ya kombe la mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yaliyomalizika mwezi Disemba mwaka jana kwenye viwanja vya shule ya Black Rhino iliyopo Arusha nchini Tanzania.

katika mashindano hayo Uganda waliibuka mabingwa baada ya kuifunga Tanzania bao 4-1 kwenye mchezo wa fainali za michuano hiyo iliyohusisha jumla ya timu tisa za  Burundi, Djibouti, Sudan, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Ethiopia, huku Eritrea na Rwanda wakijiondoa.

Tayari kikosi cha Ngorongoro Heroes kipo kambini Jijini Arusha tangu Januari 13 kikijiandaa kwaajili ya michuano hiyo ambapo baada ya droo ya makundi kufanyika itajua ipo kundi gani na timu zipi. Mashindano hayo yamepangwa kufanyika nchini Mauritania na yataanza mwezi Februari.

Jamhuri ‘Julio’ Kihwelu amesema sasa wanaelekeza nguvu zao kutafuta tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia.

 Julio amefanikiwa kuiongoza Ngorongoro Heroes kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika ambazo zitafanyika nchini Mauritania kuanzia Februari 14 hadi Machi 3 na timu nne zitafuzu moja kwa moja kwa Kombe la Dunia nchini Indonesia zilizopangwa kuanza Mei 20 hadi Juni 12 mwakani.

Kocha huyo alisema pamoja na kufungwa mabao 4-1 na Uganda katika mechi ya fainali, bado anawaamini vijana wake kuwa na uwezo mkubwa na watafanya maandalizi ya kina ili kufanya vizuri nchini Mauritania.