DONDOO 8 ZA MECHI: Tanzania Prisons 2-4 Geita Gold

- Mchezo wa Ligi Kuu kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Geita Gold uliochezwa leo Novemba 16 Uwanja wa Sokoine, Mbeya umekuwa mchezo wa pili msimu huu kuzalisha mabao mengi (6), huku mchezo wa kwanza ukiwa ule wa Mtibwa Sugar na Azam FC (3-4) uliochezwa Uwanja wa Manungu.
- Mara ya mwisho Tanzania Prisons kupata ushindi ilikua Oktoba 25 walipoilaza Polisi Tanzania mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Sokoine mabao yaliyofungwa na Jeremiah Juma kwa mkwaju wa penalti na Samson Mbangula akifunga bao la pili.
- Bao alilofunga Oscar Paul (Prisons) ndio bao lake la kwanza msimu huu kwenye Ligi Kuu kama ilivyo kwa Danny Lyanga, Shawn Oduro na Yusuph Kagoma wa Geita Gold.
- Kagoma anakuwa mchezaji wa Saba kujifunga hadi sasa kwenye Ligi Kuu, huku mchezaji mwingine wa Geita aliyejifunga msimu huu ni Oscar Masai katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Namungo.
- Kocha wa Geita Gold, Fredy Felix 'Minziro' ndiye kocha wa Ligi Kuu aliyekaa na timu kwa muda mrefu kuliko kocha yeyote. Alianza na timu hiyo msimu wa mwaka 2020/21 ikiwa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) sasa ikiitwa Championship.
- Kichapo cha leo kinaifanya Prisons kubaki na alama 14 katika nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu.
- Tanzania Prisons haijawahi kushinda mbele ya Geita Gold, ikifungwa michezo miwili huku ikipata sare moja katika mchezo wa kwanza zilipokutana msimu uliopita kwa sare ya bao 1-1 Uwanja wa Mandela, Sumbawanga.
- Ushindi wa Geita unaifanya timu hiyo kufikisha alama 17 na kupanda hadi nafasi ya sita kutoka nafasi ya 10.