Domayo bado auota ushindi wa Taifa Stars kwa Kenya

Muktasari:
Taifa Stars wamewaondoa Harambee Stars kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya dakika tisini kwa suluhu
Dar es Salaam. Kiungo wa Azam na Taifa Stars, Frank Domayo amesema haikuwa kazi rahisi kuvuka kiunzi kwa kuwatoa Kenya katika mashindano ya kuwania kufuzu Chan 2020.
Stars wamewaondoa Harambee Stars kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya dakika tisini kumalizika kwa timu hizo kuchoshana nguvu bila kufungana.
Domayo alisema ushirikiano mzuri ikiwa ni sambamba na kuamini wanaweza kuwatoa Wakenya katika mashindano hayo na kuweka wazi kuwa nafasi waliyoipata wataipambania lengo ni kuona wanafuzu hatua hiyo.
"Sare tuliyoipata nyumbani ilitupa nguvu kuamini kuwa tunaweza kushinda hata ugenini japo haikuwa rahisi kama tulivyokuwa tunafikiria kubwa tunamshukuru Mungu kwa hatua hiyo tuliyoingia tutapambana kuhakikisha tunaingia katika rekodi nyingine ya kufuzu Chan," alisema.
"Ushindi tulioupata ni wa Watanzania wote tunaposhindwa pia tunashindwa wote tunaomba ushirikiano uliotolewa katika michezo yetu yote miwili nyumbani na ugenini uendelee katika hatua tunayofuata ili kuweza kusongesha timu yetu mbele," alisema Domayo.