Dodoma Jiji yasaka rekodi

DODOMA Jiji haitanii, kwani imesisiiza kuwa wanaitaka nafasi ya nne ya Ligi Bora ili kuweka rekodi kama iliyowahi kuwekwa na KMC na Namungo ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa.

Namungo na KMC ni timu zilizoweka rekodi ya kumaliza ligi katika nne bora zikitoka kupanda daraja na kukata tiketi ya CAF kwa mara ya kwanza, KMC ikiishia raundi ya kwanza 2019 na Namungo msimu ulipopita wakitinga makundi zote zikicheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Msimu huu vita ya Nne Bora imekuwa kubwa ikihusisha timu sita zikiwa Dodoma yenye pointi 42 sawa na Namungo, Biashara United yenye 46, KMC, Polisi Tanzania (kabla ya mechi yao ya jana) na Tanzania Prisons kila moja ikiwa na alama 41.

Dodoma imebakiza mechi tatu dhidi ya Gwambina, Mtibwa na Yanga na kama itashinda zote itafikisha pointi 51 na kocha wake, Mbwana Makatta alisema ushindi wa bao 1-0 katikati ya wiki hii dhidi ya KMC imewaongeza morali kubwa ya kufanya vizuri katika mechi tatu ziliozabaki.

Makatta alisema anaamini nyota wake wataendelea kucheza ka kiwango bora wanaweza kushinda mechi zote zilizobaki licha ya kwamba si kazi rahisi, ili kutimiza lengo lao la kushiriki kimataifa.

“Tunapambana kuhakikisha malengo yetu ya kumaliza nafasi ya nne za juu yanatimia. Upinzani wa nafasi hiyo ni mkubwa kwani timu nyingi zinaitaka, ila tutapambana kwa uwezo wetu kwa mechi zilizobaki kisha kuona tunamaliza nafasi ipi, ila tunataka tiketi ya CAF,” alisema kocha huyo.

Hata hivyo, kocha msaidizi wa KMC, Habibu Kondo, alisema licha ya kipigo bado wana nafasi ya kumaliza msimu katika Nne Bora, huku kocha wa Biashara, Patrick Okumu alisema ushindani wa nafasi ya nne ni mkubwa ila hawatakubali kutoka nafasi hiyo hadi mwisho wa msimu.

“Nimekuja hapa timu hii ikiwa nafasi ya nne na malengo yetu ni kumaliza katika nafasi hiyo, hivyo lazima tuhakikishe tunatimiza dhamira hiyo na hatutaki tushuke katika hiyo nafasi hiyo, ingawa lazima tupambane “ alisema Okumu.