Dodoma Jiji yamaliza kazi, wanakuja kivingine

Wednesday September 15 2021
dodoma pic
By Matereka Jalilu

KAMBI ya siku 14 waliyoweka Dodoma Jiji mkoani Morogoro, imefikia mwisho wake kwa timu hiyo kurejea rasmi Jijini Dodoma tayari kujiwinda na ligi kuu.

Kambi hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kuiweka timu kwenye utulivu zaidi, imekamilika kama ilivyopangwa, ambapo sasa wapo tayari kwa mikikimikiki ya ligi kuu itakayoanza Septemba 27.

Timu hiyo imerejea jana Jumanne usiku kutokea Morogoro, ambapo katibu mkuu Fortunatus Johnson, ameliambia Mwanaspoti kuwa, kuvunja kambi hiyo ni mwanzo wa kujiweka tayari kuanza kwa mechi zao za ligi kuu.

Johnson aliongeza kuwa, wamerudi Dodoma ili kumalizia maandalizi hususani ya mechi tatu za kirafiki kabla ya mchezo wao wa kwanza wa ligi kuu, pamoja na ule utakaofuata dhidi ya Simba.

"Tumevunja rasmi kambi yetu Morogoro na baada ya kurudi Dodoma walimu wamehitaji mechi tatu za kirafiki kabla ya mchezo wetu dhidi ya Ruvu Shooting na Simba" alisema Johnson.

Mbali na hilo, Katibu huyo amefichua kuwa wanatarajia kuwa na mdhamini rasmi wa jezi za msimu ujao watakayemtangaza Septemba 20 na kuzinduliwa siku mbili mbele.

Advertisement

"Msimu huu tunatarajia kuwa na mdhamini rasmi wa jezi zetu ambaye ndiye atakuwa anashughulika na ishu zote za jezi kwa timu yetu" aliongeza Katibu.

Advertisement