Djuma aipigia saluti Simba

KOCHA Mkuu wa Dodoma Jiji, Masoud Djuma amesema kupoteza dhidi ya Simba halikuwa jambo la kushangaza kwao kutokana na jinsi ambavyo walikuwa na ratiba ngumu kabla ya kucheza mechi hiyo. 

Juzi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dodoma Jiji ilikubali kipigo cha mabao 3-0 ikiwa ni mechi ya raundi ya tano ya Ligi Kuu Bara.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Djuma alisema walitumia siku mbili kusafiri tangu walipocheza mechi ya mwisho, hivyo hawakuwa na muda wa kutosha kufanya mazoezi na kupumzika kwa wachezaji wake ndio maana kipindi hawakucheza vizuri.

Alisema watakuwa na mapumziko ya siku mbili kisha watakuwa na siku saba ngumu kwa wachezaji wake kufanya mazoezi ya aina tofauti kulingana na makosa yaliyoonekana kabla ya kukutana na Ihefu.

“Ihefu ni aina ya wapinzani ambao tunalingana levo moja, tunatakiwa kwenda kupambana ugenini tukishindwa kupata ushindi basi hata pointi moja itakuwa na faida kwetu tofauti na Simba iliyotuacha maeneo mengi.

“Bado tuna kazi ngumu ya kufanya hatujaanza ligi vizuri kama vile ambavyo tulikuwa tunahitaji ila naamini usikivu na kujituma kwa wachezaji wangu inawezekana tukabadili upepo huu wa matokeo.”

Masoud ameiongoza Dodoma Jiji kushika nafasi ya 11 ikiwa na pointi tano baada ya kushinda mechi moja, sare mbili na vipigo vitatu huku wakifunga mabao matatu na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara nane.