Dina atwaa medali tatu za dhahabu

Berlin, Ujerumani. Mchezaji Dina Asher-Smith amejiandikia historia kwa kutwaa medali tatu ya dhahabu kwenye mashindano ya Ulaya ‘European Championships’ akiiongoza Uingereza kushinda mbio za kupokezana vijiti za mita 4x100, mjini Berlin, Ujerumani.

Awali mwanariadha huyo mwenye kasi, alitwaa medali za dhahabu katika mbio za mita 100 na 200 kwa upande wa wanawake.

Mwanariadha mwingine wa Uingereza, Laura Muir alitwaa medali ya dhdhabu baada ya kuibuka mshindi wa mita 1500, zikiwa mbio zake za kwanza za nje huku Laura Weightman akishinda medali ya shaba baada ya kuwa wa tatu.

Nyota mwingine wa Uingereza, Eilish McColgan, alishinda medali ya fedha kwa wanawake katika mbio za mita 5,000.

Kwa ujumla siku Jumapili wanariadha wa Uingereza walitwaa medali 18, saba zikiwa za dhahabu, tano za fedha na sita za shaba na timu hiyo kuwa ya pili kwa ujumla ikijikusanyia medali 74, dhahabu 26, fedha 26 na shaba 22.

Mshindi wa jumla wa mashindano hayo ya ubingwa wa Ulaya 2018, ni Russia, ambayo ilizawadiwa medali katika hafla iliyofanyika eneo la George Square, mjini Glasgow.