Dilunga apewa mwaka Simba

Muktasari:

  • Awali, Dilunga alikuwa anatajwa kujiunga na JKT Tanzania kutokana na ukaribu wake na bosi wa juu wa timu hiyo, lakini mabosi wa Simba hawakuwa tayari kumuachia kutokana na huduma yake nzuri aliyoitoa awali.

SIMBA imekamilisha usajili wa aliyekuwa kiungo wao, Hassan Dilunga baada ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongezewa.

Awali, Dilunga alikuwa anatajwa kujiunga na JKT Tanzania kutokana na ukaribu wake na bosi wa juu wa timu hiyo, lakini mabosi wa Simba hawakuwa tayari kumuachia kutokana na huduma yake nzuri aliyoitoa awali.

Dilunga, ambaye anamudu vyema kucheza kama kiungo mshambuliaji, alipata majeraha ya goti akiwa na Simba msimu uliopita na timu hiyo haikumuongezea mkataba pale ulipomalizika.

Kiungo huyo ambaye baada ya kuwa mchezaji huru aliwahi kuonekana akifanya mazoezi ya gym kwenye klabu ya Azam FC, lakini baadaye alipoanza mazoezi ya uwanjani mara nyingi alikuwa akifanya na JKT Tanzania.

Katika kujiridhisha na mchezaji huyo, Simba ilimpa nafasi ya kufanya naye mazoezini ili kocha atakaporidhishwa na kiwango chake aweze kumsajili kwa ajili ya msimu ujao.

Mmoja wa watu wa karibu na mchezaji huyo amelithibitishia Mwananchi kwamba Dilunga tayari ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja na ndiyo maana ameanza mazoezi.

"Kweli alikuwa na dili la kwenda JKT Tanzania na pale ni kama nyumbani kwake kwa sababu walimlea tangu anaanza soka la ushindani, lakini mwisho wa siku waajiri wake wa zamani (Simba) wameona wamrejeshe," kilisema chanzo hicho.

Msemaji wa Simba, Ahmed Ally alipoulizwa alisema Dilunga amerejea kwenye kikosi chao kwa sasa ili kuangaliwa na kocha na kama akifurahishwa na kiwango chake atasajiliwa.

"Ndiyo, hii ni mara yake ya pili, lakini ni muendelezo kwake kwa sababu kuna muda huwa anaacha pale tunapokuwa tuna maandalizi ya mechi kama ilivyokuwa kwa Wydad.

"Kwa sasa amerejea kwa sababu tunafanya mazoezi kwa muda mrefu ili tucheze mechi, ndiyo sehemu ambayo kocha anazidi kumuangalia kwa mara nyingine," alisema Ally.
Dilunga alidumu Simba kwa misimu minne mfululizo, akibeba taji la Ligi Kuu mara nne na Kombe la FA (ASFC).