Dili la Bwalya laingia dosari Pamba Jiji

Muktasari:
- Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata zinadai kiungo huyo hakuwa mkweli kwa uongozi wa Pamba kwa kile alichoueleza amemaliza mkataba na Napsa Stars FC aliyojiunga nayo Agosti 31, 2024, jambo linaloleta shida ya kuja nchini kujiunga na timu hiyo.
DILI la aliyekuwa kiungo wa Simba, Mzambia Larry Bwalya la kujiunga na Pamba Jiji msimu huu limeingia dosari baada ya nyota huyo kudaiwa bado ana mkataba wa miaka miwili na Napsa Stars inayommiliki, licha ya kukiri yupo huru.
Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata zinadai kiungo huyo hakuwa mkweli kwa uongozi wa Pamba kwa kile alichoueleza amemaliza mkataba na Napsa Stars FC aliyojiunga nayo Agosti 31, 2024, jambo linaloleta shida ya kuja nchini kujiunga na timu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji wa Pamba, Peter Juma Lehhet, alisema ni kweli kumekuwa na shida ya usajili wa mchezaji huyo, japo wanaendelea kupambana na sakata hilo taratibu, huku wakiendelea na maboresho ya nyota wengine wapya.
“Jambo lake tunaendelea kupambana nalo taratibu kwa sababu zilizojitokeza, licha ya hayo ila tunaendelea na maboresho ya nyota wengine wapya ili kuhakikisha tunatengeneza kikosi imara kitacholeta ushindani mkubwa msimu ujao,” alisema Peter.
Mwanaspoti linatambua, kwa sasa uongozi wa Pamba unazungumza na wawakilishi wa Napsa Stars ili kuangalia namna nzuri ya kutatua changamoto iliyopo, baada ya Bwalya kusaini mkataba mwingine wakati bado hajamalizana na timu inayommiliki pia.
Bwalya alitua nchini kwa mara ya kwanza na kujiunga na Simba Agosti 15, 2020, akitokea Power Dynamos ya Zambia, aliyoitumikia hadi Julai 1, 2022, kisha kutua AmaZulu na baadaye Sekhukhune United zote kutoka Afrika ya Kusini.
Baada ya hapo, Bwalya alirejea kwao Zambia na kujiunga na Napsa Stars aliyoitumikia kuanzia Agosti 31, 2024 hadi sasa, kisha kusaini Pamba mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine, jambo ambalo limeleta shinda nyingine.
Pamba iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kupita miaka 23 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, imemaliza msimu wa 2024-2025, ikiwa nafasi ya 11 na pointi zake 34, ikishinda mechi nane, sare 10 na kupoteza 12, kati ya 30, iliyocheza.