Dili jipya Simba unyama sana

Dili jipya Simba unyama sana

SIMBA imepiga unyama mwingi sana jana ikifanya kufuru kwa kuingia mkataba wa kibabe wa miaka mitano na Kampuni ya M-Bet wenye thamani ya zaidi ya Sh26 bilioni.

Katika mkataba huo, Wekundu Msimbazi wataogelea mihela huku kila mwaka watavuta ongezeko fulani nono kabisa.

Mkwanja wa mkataba huo umegawanywa kwa miaka mitano ambapo kutakuwa na kiasi tofauti kila mwaka. Mwaka wa kwanza Simba itavuta Sh4.6 bilioni, mwaka wa pili itapewa Sh4.9 bilioni, mwaka wa tatu Sh5.2 Bilioni, wa nne Sh5.5 bilioni na mwaka wa tano ni Sh5.8 bilioni.

Katika pesa hiyo, Simba ilitanguliziwa Sh400 milioni kwa ajili ya usajili wa nyota wapya wa msimu ujao.

Akizungumzia mkataba huo, Mkurugenzi wa Masoko wa M-Bet, Allan Mushi alisema kusaini mkataba wa kuidhamini klabu hiyo haikuwa kazi rahisi.

Alisema iliwachukua muda mrefu kukubaliana baadhi ya vipengele kwani vipo ambavyo Simba ilikuwa inavitaka na vingine wao walikuwa wanataka vikae sawa.

“Tupo Simba kutokana na mafanikio yao kwenye Ligi ikichukua ubingwa na kufanya vizuri nje kuitangaza Tanzania, sisi pia hatupo Tanzania pekee na ndio maana tukaona tuweke nguvu hapa.

Baada ya mkataba huu tunaweza tukaendelea kuwa hapa kwa sababu sisi na Simba tunafanana hadi rangi,” alisema

Naye Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez alisema kitendo cha kampuni hiyo kuidhamini Simba ni kikubwa na kimezingatia thamani yao.

Alisema M-Bet ni kampuni kubwa ya kubeti Tanzania na imewekeza katika klabu kubwa Tanzania na Afrika Mashariki na ndio maana wamesaini mkataba huo.

“M-Bet imekidhi mahitaji yetu, huwezi kuona wanaenda sehemu nyingine kuweka udhamini katika klabu za hapa. Mkataba wetu na M-Bet ni upande wa timu ya wakubwa tu, timu za vijana na wanawake hauhusiani, labda kama tutafungua ukurasa mpya,” alisema na kuongeza:

“Wadhamini wetu wote wanne wamejipanga vilivyo kuisapoti timu yetu ndani na nje ya nchi.”

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema; “Kabla ya msimu kumalizika wadhamini wetu walitutangulizia Sh400 milioni ambazo zilikuwa ni kwa ajili ya usajili huu unaoendelea.”

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alitamba kuwa klabu yao haiwezi kufananishwa na klabu nyingine kuanzia msimu ujao.

“Zile zama za kuwa na mikataba sare sare imeshapita, sisi Simba tunahitaji vitu vya tofauti kwa sababu tumewekeza kwa kiasi kikubwa,” alisema Ahmed.

Simba na Yanga miaka ya nyuma zilikuwa zinadhaminiwa na mdhamini mmoja hivyo mikataba yao ilikuwa ikifanana katika baadhi ya mambo.

Simba inajiandaa na tamasha lake Simba Day ambalo msimu wake wa 13 umeshazinduliwa juzi na utafikia kilele chake Jumatatu ya Agosti 8.

Mastaa kibao akiwamo Zuchu kutoka lebo kubwa ya muziki nchini ya WCB, watatumbuiza katika tamasha hilo litakalofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.