Diarra aibeba Yanga mapemaa
YANGA inashuka ugenini leo dhidi ya Real Bamako, lakini wenyeji walipanga kitu flani cha kuwaharibia utulivu lakini fasta kipa Djigui Diarra akajivika mabomu na kuibeba Yanga kwa kuzipangua hujuma zote akiutumia uenyeji wa nchini humo.
Iko hivi. Real Bamako iliipa Yanga uwanja wa nyasi bandia kufanyia mazoezi ya siku mbili kabla ya jana kufanyia mazoezi yao uwanja wa mchezo.
Makocha wa Yanga walishtukia kitu kuwa uwanja huo ungewaathiri wachezaji wao hasa baada ya kujua uwanja wa Machi 26 utakaotumika kwenye mchezo ni wa nyasi za kawaida.
Diarra ambaye ni raia wa nchi hiyo kama ilivyo kwa beki Mamadou Doumbia akapiga simu moja tu kwa mabosi wa klabu yake ya zamani ya Stade Malien, kisha ikawaruhusu Yanga kwenda kuutumia uwanja wao wa mazoezi ambao una nyasi za kawaida.
Haikuishia hapo tu Yanga ikapata na mashabiki zaidi ambao waliibuka kwa wingi kumsalimia Diarra ambaye amekuwa na mafanikio zaidi tangu atue timu hiyo.
Yanga ilipotua uwanja wa ndege tu, mapokezi ya kipa huyo yalikuwa ya kuvutia kwa kila shabiki kumsaka na kumshangilia kila walipomuona.