Demba Ba aizamisha Man United

Demba Ba jana
CHELSEA, ENGLAND DEMBA Ba jana, Jumatatu aliibuka shujaa baada ya kuifungia Chelsea bao tamu katika mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la FA dhidi ya Man United. Ba alifunga bao hilo dakika ya 49 kwa kuuwahi mpira wa juu uliopigwa na Juan Mata na kuuzamisha wavuni kwa mguu wa kulia huku akimuacha kipa wa Man United, David De Gea katika hali ya mshangao asijue la kufanya baada ya kupotea maboya. Matokeo hayo yanaifanya Man United kuiaga michuano hiyo baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kwanza kwenye uwanja wao wa nyumbani huku Chelsea ambao ndio mabingwa watetezi wakisubiri kuvaana na Man City katika mechi ya nusu fainali hapo Aprili 14 wakati Millwall itaumana na Wigan katika nusu fainali nyingine itakayochezwa Aprili 13. Man United nusura isawazishe bao hilo dakika chache baada ya kufungwa baada ya Javier Hernandez kuunganisha mpira kwa kichwa akiwa karibu na lango la Chelsea lakini kipa Petr Cech alikuwa makini na kuutoa mpira huo uliokuwa ukielekea golini. Chelsea: Cech, Ivanovic, Cole/Bertrand, David Luiz, Azpilicueta, Ramires, Mata, Oscar/Moses, Mikel, Hazard na Ba/Torres. Man United: De Gea, Evra, Jones, Ferdinand, Smalling, Valencia, Carrick, Nani/Giggs, Cleverley/Van Persie, Hernandez, Welbeck/Young.