Dejan apewa ujanja

DEJAN Georgijevic wa Simba ameendelea kuwa gumzo kwa mashabiki wa soka. Baadhi wakimponda kwa kiwango alichokionyesha hadi sasa akiwa na timu hiyo, lakini nyota wa zamani wamempa akili straika huyo Mserbia wakisema akitupia nyavuni na kuwa na mwendelezo atawafunga watu midomo.

Dejan mwenye bao moja katika Ligi Kuu Bara, kumbe hata yeye amekuwa akizisikia kejeli na mijadala juu yake na kusema, anaamini wanaomcheka leo ndio watakaomshangilia kwani anakiamini kiwango chake na kushindwa kutupia wavuni hutokea kwa mchezaji yeyote kutokana na presha kubwa.

Tuanze na wadau, inaelezwa straika Dejan akiwa na mwendelezo wa kucheka na nyavu, atawafanya mashabiki wamsahau Meddie Kagere aliyeacha rekodi ya mabao 65 ndani ya misimu minne kabla ya kuachwa msimu huu na kutua Singida Big Stars.

Kagere alijunga na Simba 2018/19, akitokea Gor Mahia ya Kenya na kufunga mabao 23 na msimu uliofuata alifunga 22 na mara zote alibeba tuzo ya Mfungaji Bora na msimu wake wa tatu alifunga mabao 13 kisha msimu uliopita alifunga saba kabla ya kutemwa kikosini


sambamba na Chris Mugalu aliyepo Iraq kwa sasa na Taddeo Lwanga aliyesajiliwa AS Arta Solar 7 ya Djibouti.

Ujio wa Dejan kikosini ulitazamwa kama unaenda kuziba nafasi ya Kagere, jambo ambalo wadau wa soka wamelizungumzia wakimtaka awe na mwendelezo wa kufunga ili kuwaaminisha mashabiki kupata mtu wa mabao.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema mchezaji kuondoka kwenye timu na kuja mwingine sio dhambi, isipokuwa anayekuja kuziba pengo anapaswa kujua aliyekuwepo alikuwa na mchango gani.

“Mfano kuna nyakati Emmanuel Okwi alikuwa anaimbwa kila wakati, alipokuja Kagere akauzima ufalme wake na kuwafuta machungu mashabiki, hilo ndilo linalotakiwa alifanye Dejan ili ajijengee ufalme wake ndani ya Simba nje na utani unaomfanya ajulikane,” alisema Ulimboka.

Kocha mkongwe na nyota wa kimataifa wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni, alisema Dejan ana deni kwa mashabiki kufanya kile wanachokitarajia kutoka kwake, ili waanze kuamini uwezo wake kama utaibeba timu.

“Hakuna mchezaji anayeweza kuchukiwa kama anafanya vitu vya kuibeba timu yake, mfano wakati anasajiliwa Joash Onyango wengi walimuona kama mzee, lakini akafanya kazi iliyobadilisha mtazamo huo na akawa nguzo muhimu kwenye timu,” alisema Kibadeni, huku Mohamed Banka kiungo fundi wa zamani wa kimataifa aliyezitumikia Simba, Yanga na Moro United alisema hakuna namna nyingine ya mchezaji kuwafurahisha mashabiki wake zaidi ya kufanya majukumu yake kikamilifu.

“Siyo Dejan pekee bali hata Habibu Kyombo anapaswa kupambana sana, ili kuonyesha viongozi hawakukosea kumsajili, hivyo wanatarajia ligi ikianza wafanye makubwa na shida za klabu kongwe ni utani,” alisema Banka aliyecheza soka Zanzibar na Bandari ya Kenya.


MSIKIE DEJAN

Straika huyo alisema kwa muda aliopo katika kikosi hicho amebaini ni moja ya timu nzuri ambayo inaweza kushinda mechi nyingi katika mashindano tofauti na hamu yake ni kuona anaipa mafanikio makubwa ikiwamo kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ASFC na kufika mbali mechi za CAF.

Alikiri ni kweli baada ya kufunga katika mechi ya ligi dhidi ya Kagera Sugar na kupata muda wa kucheza mechi za kirafiki Sudan presha kwake imepungua sio kama ilivyokuwa hapo awali.

“Naimani hali hiyo ya kujiamini niliyokuwa nayo wakati huu itakwenda kunisaidia na kuweza kufunga zaidi katika michezo mingine iliyokuwa mbele yetu katika mashindano yote,” alisema Dejan na kuongeza;

“Jambo muhimu ni kushinda mechi nyingi za ligi ili kukusanya pointi nyingi, ili kufanikisha hilo kwa upande wangu natakiwa kupambana na kucheza vizuri kila mechi na kufunga. Baada ya kucheza mechi moja ya ligi tutakuwa na mchezo mgumu ugenini wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi tunahitaji kuanza vizuri .”

Dejan alisema anafahamu huko mtaani anaimbwa na kuongelewa ‘lete mzungu’ hilo, kwake wala halina shida kwani hata baadhi ya wachezaji wenzake wamekuwa wakimtania wakiwa kambini.

Alisema anawapenda mashabiki wa Simba kutokana na kuipenda timu yao zaidi katika maisha yake ya soka hajawahi kukutana na nguvu kama hiyo anayopata wakati huu akiwa na kikosi hicho. “Itakuwa si msimu wangu rahisi hapa Tanzania kutokana ndio mara ya kwanza. Ugumu wa ligi upo na ushindani ni mkali katika kila timu nilizocheza nazo na hata zile nilizopata nafasi ya kuziona kupitia runinga,” alisema Dejan na kuongeza;

“Hata kama nitaenda kucheza katika viwanja vyenye mazingira magumu na kukutana ushindani wa kutosha huko nitajitahidi kuonyesha kiwango bora na kuisaidia timu kupata matokeo mazuri,”

“Naamini kila changamoto iliyokuwa mbele yangu nitaizoea na baada ya hapo nitakuwa na njia sahihi na kuitatua ili kuona natoa mchango kwa timu timu kutimiza majukumu ya nafasi yangu.”