De Gea, Neuer waisahaulika tuzo ya dunia

Muktasari:

  • Makipa hao wamekuwa katika kiwango cha juu lakini wameshindwa kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka

Mwaka 2012 pale Allianz Arena nilimwona Manuel Neuer akipigiwa Saluti na zaidi ya watu 65,000. Hiyo ndiyo Heshima kubwa wajeruman walimzawadiwa kabla hajawazawadia Kombe la dunia.

Mwaka 2014 Thiey Henry alipofungua bahasha yenye Maneno kwamba Cristiano Ronaldo ndiye mchezaji bora wa dunia.

Nakumbuka kazi yake akiisaidia timu ya taifa kwenye kombe la dunia mwaka 2014. Mikono yake ilikuwa na thamani kubwa kuliko miguu ya Ronaldo na Messi mwaka ule. Aliokoa michomo 23 kwenye michezo 7 ya kuipigania taifa lake.

Lakini nani anayejali mikono ya makipa? Soka ni mpira wa miguu sawa lakini je hatuoni thamani ya mikono ya De gea kweli? Kazi ya mikono kwenye soka ni sawa na nguo za ndani kwa dada zetu wa daslam sio kitu cha muhimu sana kwa kizazi hiki, watakwambia tatizo joto.

Wanapigiwa mashuti na akina Steven Gerrard na Alex kama wanataka kuwaua na wanaruka kuyafuata  bado watu hawaoni thamani yao? Kosa moja la goli kipa linaweza kuigharimu timu nzima. Leo hii goli kipa wa Real Madrid akikosea wakafungwa fainali ya UEFA Ronaldo hana ballon D or hata kama akifunga magoli 100.

 Goli kipa wa Barcelona akicheza vizuri akatwaa UEFA hata kama Messi amefunga magoli mawili fahamu fika Messi ana nafasi ya kutwaa Ballon D Or kuliko Ronaldo Mwenye magoli 100. Msaada wa mkubwa wa magolikipa umetumika kama tishu ya kuwafanyia usafi washambuliaji.

Kuna baadhi ya mashuti Golikipa akiokoa ni sawa tu na mchezaji aliyefunga goli. Kama huamini waulize Arsenal wanajisikiaje nafasi 14 zilizochomolewa na De gea. Hebu jaribu kutazama kazi ya akina De gea vizuri.

 Kujirusha kwenye zile nguzo za chuma kama chizi sio kazi rahisi hata kidogo. kama huamini mwambie Messi akadake. Mabeki wakiwa wanazuia ukuta wa mpira wa adhabu huwa wanazuia nini na mikono? Kwanini wanaficha maeneo hayo? Je makipa wakiwa golini wanazuia kitu? Golikipa ana kazi ya kujitoa muhanga hata kuuachia uso wake na sehemu nyingine nyeti ilimradi tu Kwenye vyumba vya kubadilishia nguo asitukanwe na Mourinho.

Zipo timu kama sio makipa wao leo hii wangekuwa mtaa wa 7. Sijataja timu yeyote samahani. Msimu huu nitashangaa sana kama De Gea hatopewa mchezaji bora wa msimu. Najua watu waliverpool mtataka kunipiga mawe kwa sababu mnaamini Salah anastahiki.

Kipa wahesabiwe mechi ambazo hawajafungwa, mashuti aliyokoa, namna wanavyopanga safu yao ya ulinzi, staili zao za uokoaji (Kama Neuer unashindwa kuelewa ni beki au kipa), penati walizookoa nakadhalika. Kwa mtazamo wangu, kama FIFA hawaoni umuhimu wa mikono basi watumie miguu kula nayo chakula. Golikipa ana kazi ya kuwazuia wachezaji 10 wasimfunge na wakati mwingine mpaka 11 maana akina Lukaku wanaotaka kujifunga nao wapo wengi.

Kwangu mimi Degea ni mchezaji bora wa dunia hii hii ambayo vyuma vimekaza. Zile tuzo zao wanazotoa kisa eti mtu kabeba sijui kombe gani waendelee kugawana tu.

De gea hajawahi kuwa hata  mchezaji bora wa ligi sioni kama atatwaa Ballon D Or labda hiyo tuzo itolewe Masasi au Rombo? Mwenzake Neuer kashakuwa mchezaji bora wa UEFA mara 5, mchezaji bora wa Bundasliga mara 2 na aliishia kuwa mchezaji bora namba 3 mkononi akiwa na kombe la dunia lakini hola. Wewe De Gea nenda tu mkafarijiane na Neuer vyuma vimekaza na girisi wanayo washambuliaji.