Dante aibuka upya Yanga  

ALIYEKUWA beki wa Yanga, Andrew Vicent ‘Dante’ ameikalia kooni klabu hiyo baada ya kuweka wazi kwamba bado kuna sehemu ya pesa zake za usajili anaidai.

Akipiga stori na Mwanaspoti, Dante alisema sehemu ambayo anadai ni pesa yake ya usajili Sh32 milioni ikiwa ni ya mkataba wa miaka miwili uliokuwa na thamani ya Sh50 milioni.

Dante alisema awali alipewa sehemu ya pesa yake alipomaliza mkataba na kukaa chini na viongozi wa Yanga ili kulipwa stahiki zake ndipo alipokumbana na changamoto ya kutakiwa kukatwa baadhi ya fedha.

“Baada ya kumaliza mkataba na kwenda pale klabuni kwa ajili ya kujua tunaachanaje vizuri, ndipo waliniambia kwamba hela yangu inakatwa, nilipohoji walisema kuna vitu walikuwa hawakati ndio maana natakiwa nikatwe,” alisema mchezaji huyo.

“Nilihoji kwaninini haikuwa hivyo awali na kwanini hawakuniambia, basi sikuchukua kile ambacho walitaka kunipa na kwa sababu mimi najua pesa yangu ni nyingi kuliko kile ambacho wanataka kunipa mpaka sasa.”

Beki huyo aliongeza kuwa tayari ameshaanza taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba anapata stahiki zake zote zilizosalia katika kikosi hicho cha Jangwani.

Mwanaspoti halikuishia hapo, bali liliwatafuta viongozi wa Yanga na ofisa habari wa timu hiyo, Hassan Bumbuli alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alisema hawezi kuzizungumzia mpaka awe ofisini.

“Nilikuwa katika msiba wa mke wa (Bakari) Mwamnyeto, kulikuwa na mvua nyingi sana kule na tukarudi nyumbani usiku sana, kwa hiyo hizo taarifa ni mpaka niingie ofisini,” alisema Bumbuli licha ya Mwanadpoti kufahamu kwamba suala hilo lipo ofisini kwao muda mrefu sasa.

Ikumbukwe kwamba Dante mwanzoni mwa msimu uliopita aligoma kuichezea timu hiyo akidai pesa zake za usajili pamoja na malimbikizo ya mishahara, lakini baadae alipewa Sh15 milioni na kurejea katika kikosi hicho ambapo pia hakupata nafasi ya kucheza.

Inaelezwa kwamba Dante alisaini na Yanga mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh 50 milioni.

Kwa sasa beki huyo ambaye kabla ya kukwaruzana na uongozi wa Yanga aling’ara kikosi, anaichezea KMC ya Kinondoni.