Dalali: Tukifanya haya mwarabu hatoki

Muktasari:
- Dalali ambaye uongozi wake unakumbukwa kwa kuanzisha tamasha la Simba maarufu kama Simba Day, alisema jambo la kwanza ni viongozi kuendeleza mshikamano ambao wamekuwa nao tangu msafara wa timu hiyo ulipotua Morocco.
MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Hassan Dalali amesema hadi sasa maandalizi ya timu hiyo kwa mchezo wa ugenini wa hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco ni mazuri na anaamini timu yake itapata matokeo mazuri ikiwa itafanya baadhi ya mambo.
Dalali ambaye uongozi wake unakumbukwa kwa kuanzisha tamasha la Simba maarufu kama Simba Day, alisema jambo la kwanza ni viongozi kuendeleza mshikamano ambao wamekuwa nao tangu msafara wa timu hiyo ulipotua Morocco.
“Nimefurahi kuona viongozi wamekuwa wakipeana ushirikiano sana katika kushughulikia masuala ya timu. Kama tukiendelea hivi, nina imani tutamfunga Berkane nje na ndani,” alisema Dalali.
Aliongeza wachezaji na benchi la ufundi wanapaswa kucheza kwa nidhamu kubwa na wasikubali kuvurugwa kisaikolojia na changamoto zozote za nje ya uwanja.
“Waarabu huwa wana mbinu nyingi za kuwatoa mchezoni wachezaji wa timu pinzani hasa katika mechi muhimu na kubwa kama hii ambayo tunacheza nao. Kama ukiingia katika mtego wao tu, umekwenda na maji," alisema Dalali na kuongeza;
“Hivyo niwasihi wachezaji wetu pamoja na makocha wasiweke akilini kabisa masuala yote ambayo yanatokea na yatatokea nje ya uwanja na badala yake akili waielekeze kwenye mchezo tu ili tupate matokeo mazuri.
“Kama timu nzuri tunayo na wachezaji wakiwa na utulivu, mimi nina imani kubwa tutachukua hili kombe kama ambavyo Wanasimba wote tunaamini kutokana na ubora wa timu yetu,” alisema Dalali.
Dalali alisema, kila Mwanasimba anapaswa kuitazama mechi hiyo kama vita hivyo aingie katika uwanja wa mapambano kuhakikisha Simba inaipa heshima Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.