Dabo apendekeza msaidizi Azam FC

Muktasari:

  • Dabo raia wa Senegal alitambulishwa rasmi kuifundisha timu hiyo Mei Mosi mwaka huu akichukua nafasi ya Kali Ongala ambaye anaendelea kusimamia hadi mwisho wa msimu huu.

KOCHA mpya wa Azam FC, Youssouph Dabo amependekeza kupatiwa msaidizi wake ndani ya timu hiyo atakayeshirikiana naye wakati atakapoanza majukumu msimu ujao.

Dabo raia wa Senegal alitambulishwa rasmi kuifundisha timu hiyo Mei Mosi mwaka huu akichukua nafasi ya Kali Ongala ambaye anaendelea kusimamia hadi mwisho wa msimu huu.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo ililiambia Mwanaspoti, Dabo anataka kuleta watu wa kufanya naye kazi ambao anaamini watamsaidia katika kutimiza malengo ya klabu.

"Ni moja ya mapendekezo yake ya kupatiwa msaidizi lakini bado suala hilo halijaamuliwa kwa viongozi ingawa bado muda upo wa kutosha hivyo tusubiri kuona nini ambacho kitatokea japo kuna uwezekano akapewa mahitaji anayotaka ili kurahisisha utendaji kazi wake," kilisema chanzo hicho.

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin 'Popat' alisema kwa sasa wako kwenye maandalizi ya kumalizia msimu na baada ya hapo wataendelea na programu za msimu ujao hivyo mambo yote yanayohusu mabadiliko kwenye benchi la ufundi yatajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi baadae.

Hata hivyo Mwanaspoti linatambua endapo Dabo ataletewa msaidizi haitoweza kuathiri nafasi ya Kali Ongala kwani kocha huyo ataendelea na majukumu yake ya kocha wa washambuliaji.
Dabo ametua kwenye timu hiyo baada ya kuachana na ASC Jaraaf de Dakar huku akikumbukwa zaidi baada ya kuifundisha Teungueth iliyokuwa na staa wa Simba, Pape Sakho na Malikcou Ndoye wa Azam.