Dabi ya Kariakoo ni mtego

Muktasari:

  • Ingawa kwa mujibu wa wazoefu ambao ni makocha na wachezaji wakongwe, takwimu huwa hazihusiki au haziamui sana inapofika kwenye dakika 90 za dabi lakini kilichopo sasa, takwimu za mechi mpaka hapa ligi ilipo zinaibeba zaidi Yanga.

Kariakoo Dabi ya 112 ndani ya Ligi Kuu, inapigwa saa 11:00 jioni, Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa lakini kwa takwimu zilivyokaa kuna mtego ambao kila timu inahitaji akili ya ziada ya kiufundi kuuvuka. Vinginevyo, kuna mtu atalala na maumivu makali.

Ingawa kwa mujibu wa wazoefu ambao ni makocha na wachezaji wakongwe, takwimu huwa hazihusiki au haziamui sana inapofika kwenye dakika 90 za dabi lakini kilichopo sasa, takwimu za mechi mpaka hapa ligi ilipo zinaibeba zaidi Yanga.

Mpaka sasa ndani ya Ligi Kuu Bara, Yanga imeshuka dimbani mara 21 ikiwa kinara wa ligi hiyo, huku Simba ikicheza mechi 20 na kukamata nafasi ya tatu.

Kitakwimu, Yanga ipo vizuri katika suala zima la kufunga na kuzuia nyavu zao zisitikiswe kulinganisha na ilivyo kwa Simba ndani ya ligi msimu huu.

Simba, eneo lao la kushambulia, makali yameshuka, pia walinzi wao wanaruhusu mabao kirahisi kiasi cha kushuka dimbani mara 20 na kushuhudia nyavu zao zikitikiswa mara 19.

Kwa wastani, Simba inaruhusu bao kila mchezo jambo ambalo kama timu ni wazi kuna tatizo eneo hilo na linatakiwa kufanyiwa marekebisho, la sivyo kitawakuta kitu.

“Kuna shida eneo la ushambuliaji, hata ulinzi pia hawapo vizuri, hivyo lazima warekebishe maeneo hayo ili kuwa bora zaidi kama wenzao Yanga kama wanataka kushinda mechi hii. Umakini kila dakika ni muhimu sana, hii ni dabi,” alisema Abdallah Kibadeni Kocha na staa wa zamani wa Simba.

Jambo hilo linatoa taswira Yanga ina nafasi ya kupata bao katika mchezo huu ambao wengi wanasema siku zote huwa hauna mwenyewe mpaka mwamuzi apulize kipyenga cha mwisho.

Katika mechi 21 ambazo Yanga imecheza na kukusanya alama 55 ndani ya ligi msimu huu, imepata ushindi mara 18, sare 1 na kupoteza 2 dhidi ya Ihefu na Azam. Imefunga mabao 52 na kuruhusu 11.

Simba yenyewe imekuwa na wakati mgumu katika kushinda mechi zake ikiwa tayari imepata ushindi mara 14 kati ya 20, sare 4 na kupoteza 2 dhidi ya Yanga na Tanzania Prisons.

Wakati ikiwa na rekodi mbaya katika safu yao ya ulinzi, timu hiyo imefunga mabao 40, ikiwa ni timu ya tatu yenye mabao mengi baada ya Yanga (52) na Azam (49) kabla ya mchezo wao wa jana dhidi ya Mashujaa.

Ukiangalia takwimu za mabao kwa jumla, Yanga wachezaji wake wengi wapo kwenye nafasi za juu katika orodha ya wenye mabao mengi.

USHAMBULIAJI

Yanga wapo vizuri katika kucheka na nyavu, wachezaji wake tofauti wana mabao mengi ambapo Stephane Aziz Ki amefunga 14, Maxi Nzengeli (9), Mudathir Yahya (8) na Pacome Zouzoua (7). Hao ni wale wanaofuatana kwa ukaribu sana.

Kwa upande wa Simba, Saidi Ntibazonkiza na Clatous Chama, ndiyo wenye mabao mengi (7) kwa wachezaji waliopo sasa kikosini hapo, ingawa katika orodha, Jean Baleke ambaye ameondoka dirisha dogo, amefunga mengi zaidi (8).

Baada ya hapo, unakutana na Freddy Michael mwenye mabao matatu kama ilivyo kwa John Bocco na Moses Phiri ambaye naye aliondoka sambamba na Baleke.

Yanga katika ishu ya kufunga mabao, ina wastani wa kufunga mabao (3) kila mechi, wakati Simba wastani wao wa kufunga bao kila mechi ukiwa ni (2). 

ASISTI

Ukiachana na mabao, Yanga pia wachezaji wake namba zinawabeba katika asisti, Aziz Ki na Yao Attohoula kila mmoja anazo 7, Clement Mzize (5), Pacome na Nickson Kibabage (4).

Ukija upande wa Simba, mwenye asisti nyingi ni Clatous Chama (5), anafuatiwa na Mohamed Hussein na Shomary Kapombe ambao kila mmoja anazo 4.

ULINZI

Katika eneo la ulinzi la Yanga, ukiondoa mabeki, kipa wao Djigui Diarra ndiye aliyecheza mechi nyingi zaidi katika ligi msimu huu akiwa amekusanya clean sheet 9, huku timu nzima ikiwa imekusanya clean sheet 13 katika mechi 21, Simba kipa wao, Ayoub Lakred anazo clean sheet 5 kati ya 8 zilizopatikana kikosini hapo baada ya mechi 20.

Kibaden ambaye ana historia kubwa na dabi hiyo akiwa ndiye mchezaji pekee mwenye hat trick aliyoifunga mwaka 1977, amezichambua Simba na Yanga kuelekea mchezo huo akisema:

“Timu zote nimekuwa nikizifuatilia namna zinavyocheza, nimeona Yanga wapo vizuri sana kuanzia safu yao ya ulinzi hadi ushambuliaji.

Mechi zao wanavyocheza unaona kabisa kuna jambo fulani wanalitafuta na mwishowe wanalipata.

“Yanga wamekamilika, wana kikosi ambacho akikosekana mtu fulani, inakuwa kama vile hakijatokea kitu.

“Lakini upande wa Simba, kuna shida eneo la ushambuliaji, hata ulinzi pia hawapo vizuri, hivyo lazima warekebishe maeneo hayo ili kuwa bora zaidi kama wenzao Yanga.”

Kwenye makaratasi, Yanga imebakiwa na michezo tisa mkononi, ili Yanga iweze kutwaa ubingwa, katika mechi hizo, inapaswa kushinda saba na sare moja ili kufikia alama 77 ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani wake wa karibu, Azam na Simba SC.