Conte kufanya usajili wa kufuru Chelsea

Muktasari:
Chelsea tayari imeshautema ubingwa wa Ligi Kuu England kutokana na kuachwa pointi nyingi na Man City vinara wa ligi hiyo
LONDON, ENGLAND
CHELSEA wameambiwa hivi hakuna namna nyingine zaidi ya kuwarudisha kwenye makali kama si kutumia Pauni 250 milioni kwa usajili wa mwisho wa msimu.
Kocha wa timu hiyo, Antonio Conte amesema anahitaji apewe Pauni 250 milioni za kufanya usajili kwenye dirisha kubwa ili kuifanya Chelsea ya msimu ujao iwe kwenye moto mkali.
Mtaliano huyo amekuwa kwenye wakati mgumu msimu huu, Chelsea ikishindwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu England baada ya kufanya mabadiliko kwa kuleta wachezaji wanane wapya kwenye kikosi chake.
Conte alisema ili kuweza kushindana na kasi ya Manchester City, Chelsea itahitaji kusajili na si kusajili tu, bali kunasa wachezaji wenye viwango vya dunia wasiopungua watatu, ambao gharama ya pamoja inaweza kuwa Pauni 250 milioni.
Kutokana na hilo, Conte anawataka Thomas Lemar wa Monaco, ambaye anatajwa kuwa thamani yake ni Pauni 90 milioni, Antoine Griezmann wa Atletico Madrid, ambaye thamani yake ni Pauni 95 milioni na beki wa kati wa Tottenham, Toby Alderweireld, ambaye thamani yake inatajwa kuwa ni Pauni 65 milioni.
Conte, ambaye aliwahi kuinoa Juventus alisema: “Lazima tukubali ukweli, tunapaswa kupandisha kiwango chetu.
“Kwa sasa tunasumbuka kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini hilo litakuwa si tatizo tena kama tutapata wachezaji watatu wa maana na si wanane wa kawaida."