Coastal Union yampigia hesabu kocha Tabora United

Muktasari:
- Timu hiyo awali ilikuwa ikifundishwa na Juma Mwambusi, aliyeondolewa kutokana na matokeo mabaya ambayo klabu hiyo ilikuwa ikiyapata.
COASTAL Union inapiga hesabu kali za kumchukua aliyekuwa kocha wa Tabora United, Anicet Kiazayidi kushika nafasi ya Joseph Lazaro msimu ujao.
Timu hiyo awali ilikuwa ikifundishwa na Juma Mwambusi, aliyeondolewa kutokana na matokeo mabaya ambayo klabu hiyo ilikuwa ikiyapata.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Coastal, kiliiambia Mwanaspoti, mipango ya klabu hiyo sasa ni kumchukua Anicet kutokana na uwezo aliouonyesha alipokuwa Tabora kabla ya kwenda mafunzoni na kuwa mwisho wa kibarua alichokuwa nacho kwa Nyuki wa Tabora.
“Coastal inaamini kuwa, ikimpata Anicet timu hiyo inaweza kurejea kwenye ubora wake wa msimu uliopita, kutokana na kile ambacho wamekiona kwa Tabora United. Ni kocha mzuri kweli hivyo kama mabosi watafikia makubaliano, basi tutakuwa naye na mtamuona ila kwa sasa jina lake ndilo lililopo vichwani mwa matajiri hao wa Tanga,” kilisema chanzo hicho.
Mkongomani huyo aliyeipa Tabora mafanikio kabla ya kuondoka, alidaiwa kupishana na mabosi wa juu wa timu hiyo.
Kocha huyo kwa sasa hana timu yoyote anayoifundisha, hivyo huenda dili hilo la Coastal likakamilika kiulaini, kwani kocha waliyenaye hana vigezo vya kufundisha timu za Ligi Kuu. Kwa sasa timu nyingi zinazoshiriki Ligi Kuu, zimebakiza mechi mbili kumaliza msimu, huku michezo hiyo ikitarajiwa kumalizika Juni 22.
Coastal Union ambayo msimu uliomalizika ilikuwa nafasi ya nne na ikafanikiwa kushiriki michuano ya CAF, sasa iko namba 10 katika msimamo ikiwa na pointi 31 ikishinda mechi saba, sare 10 na kupoteza 11.