Clara Luvanga kiwasha kwa thibaut courtois

HATIMAYE ukimya wa aliyekuwa mchezaji wa Yanga Princess, Clara Luvanga umeibuliwa na kishindo baada ya kusajiliwa na Dux Logrono ya Hispania inayomilikiwa na kipa wa Real Madrid na timu ya taifa la Ubelgiji, Thibaut Courtois.

Clara ambaye ni mshambuliaji, amejiunga na chama hilo la Courtois ambalo lipo Ligi  Daraja la Kwanza Hispania kwa mkataba ambao utamfanya kulichezea kwa misimu mitatu.

Kupitia ukurasa rasmi wa klabu hiyo, Alhamisi iliyopita, iliposti picha yake pamoja na uju-mbe uliosema, ”Leo tuna-karibisha divai ya mvinyo kwa mchezaji  Clara Luvanga,  Mtanzania akisaini kwa misimu mitatu kwa ajili ya kuvaa jezi ya Rioja. Karibu nyumbani kwako.”

Clara ambaye yupo nchini akijiandaa na maisha yake mapya, alisema kwake ni nafasi ya kipee, ”Ninafuraha kusajiliwa na Dux Logrono, nasubiri kwa hamu kukutana na wachezaji wenzangu kwa ajili ya kupambania timu na kuwapa furaha mashabiki wetu.”

Wadau mbalimbali wa soka la Wanawake nchini wamefurahia hatua ya binti huyo wanaamini anaweza kufanya makubwa barani Ulaya na kufungua njia kwa wachezaji wengine wa kike.

“Nguvu na uwezo wake wa kufunga vitamsaidia sana kupiga hatua, sio mbaya kwa kuanzia katika Daraja la Kwanza, baada ya muda mfupi anaweza kupata ulaji kwa timu za Ligi Kuu, kikubwa ni kufanya vizuri tu,” alisema Mohammed Badru ambaye ni kocha wa timu za vijana za Azam FC.

Dux Logrono ina miaka 15 tangu kuanzishwa kwake 2008. Julai mosi 2021 iliwekwa sokoni na ndipo ikanunuliwa na DUX Gaming (ambao washirika wake ni DJMariio na wanasoka Thibaut Courtois wa Real Madrid na Borja Iglesias anayekipiga katika klabu ya Real Betis ya La Liga.