Chanongo azidi kuwa mtamu

WAKATI Straika mkongwe, Haruna Chanongo akiendeleza makali Pamba Jiji, benchi la ufundi limesema haijaisha mpaka iishe likiahidi Ligi Kuu msimu ujao ni uhakika.

Pamba imekuwa na miaka kibao bila kucheza Ligi Kuu tangu ilipotwaa ubingwa kombe la Muungano mwaka 1990 kisha kushuka daraja mwaka 2000 haijarejea tena na sasa kiu yao ni kuona mwaka huu inafanya kweli.

Straika wa timu hiyo, Chanongo juzi akiiongoza timu hiyo jijini Mbeya alifikisha mabao 10 katika sare ya 2-2 dhidi ya Ken Gold wanaoongoza ligi ya Championship.

Nyota huyo wa zamani wa Simba, Stand United, Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting anawasogelea vinara wa mabao kwenye ligi hiyo inayoongozwa na Willy Edgar (Ken Gold) mwenye 18, Boban Zirintusa (Biashara United) mwenye 16.

Wengine ni Oscar mwajanga (Mbeya Kwanza) aliye na 14 Frank sawa na Maulid Shaban wa Mbeya City, huku Francis wa TMA akiwa nayo 13 na kufanya vita kwenye ufungaji bora kuwa nzito.

Kocha wa viungo wa timu hiyo, George Aron alisema sare waliyopata dhidi ya Ken Gold inawaweka katika mazingira mazuri kupigania safari yao ya muda mrefu kucheza Ligi Kuu.

Alisema kwa sasa wanaenda kusahihisha makosa ya timu nzima kuhakikisha wanashinda mechi mbili za nyumbani dhidi ya Polisi Tanzania na FGA Talent kisha kuzifuata Mbuni na TMA Arusha.

“Tuna uhakika mechi mbili za nyumbani tutashinda na kufikisha alama 61 kisha tunaenda kufia uwanjani huko Arusha mbele ya TMA na Mbuni na kusubiri ndoto yetu ya muda mrefu” alisema Aron.