Chamungu akili ipo Ligi Kuu tu

MSHAMBULIAJI wa FGA Talents FC, Andrew Chamungu amesema malengo yake makubwa msimu ujao ni kucheza Ligi Kuu Bara.

Chamungu alisema licha ya ushindani uliopo katika ligi hiyo ila ni muda sasa mwafaka wa kujipanga kwa ajili ya changamoto za Ligi Kuu Bara ndoto anayoendelea kuiishi hadi pale atakapoitimiza akiwa na kikosi hicho.

“Jambo la kwanza ni kuisaidia timu yangu kucheza Ligi Kuu msimu ujao kwa sababu naamini inawezekana kutokana na ubora wa wachezaji wetu na ushirikiano uliopo, ni ndoto kubwa ila nitaipambania,” alisema na kuongeza;

“Hii ni nafasi nyingine kwangu ya kuonyesha uwezo wangu ambao watu wengi walikuwa wanaufahamu, hivyo jukumu langu ni kuhakikisha narudisha ile imani ya mashabiki zangu wanaonipa sapoti kwenye kila hatua ninayopiga.”

Chamungu aliyewahi kuichezea Polisi Tanzania amejiunga na kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Mbuni FC aliyoichezea kwa mkataba wa miezi sita tangu alipojiunga nayo akitokea Kitayosce.

Huu ni msimu wa pili kwa nyota huyo kuichezea tena timu hiyo baada ya kuitumikia kwa msimu uliopita ambapo tangu ajiunge nayo tayari amefunga bao moja katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting waliposhinda kwa mabao 2-1.