Chama, Saido waachiwa msala Simba

BAADA ya kulazimishwa sare ya bao 1-1, dhidi ya Azam, kikosi cha Simba kitakuwa tena kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kesho kucheza na Geita Gold katika mchezo mkali na wa kusisimua wa Ligi Kuu Bara unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka.

Wakati timu hizo zikikutana, mjadala wa muda mrefu kuhusu nani awe anapiga mipira ya kutenga (frii-kiki, kona na penalti) katika kikosi cha Simba, ambapo sasa Mzambia, Clatous Chama na Mrundi, Saidi Ntibanzokiza 'Saido' wameachiwa mpira rasmi.

Awali, kocha aliyeondoka Msimbazi, Mbrazil Roberto Oliveira 'Robertinho' alikuwa amemchagua Saido kupiga frii-kiki zote Simba itakazozipata karibu na lango la mpinzani lakini ujio wa Mualgeria, Abdelhack Benchikha umemuongeza Chama na tayari ameanza kuonyesha matunda.

Katika mechi mbili za Simba zilizopita mabao mawili kati ya matano iliyofunga timu hiyo yametokana na mipira ya kutenga, na yote yametokea kwenye miguu ya Chama.
Chama alianza kufanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Tabora United ambapo Simba ilishinda mabao 4-0, kwa kutoa asisti huku akipiga frii-kiki ambayo ilitua kichwani kwa mshambuliaji, Pa Omar Jobe na kusukuma mpira nyavuni na kuitanguliza timu hiyo.

Pia Mwamba huyo wa Lusaka, ndiye aliipa Simba pointi moja dhidi ya Azam dakika za jioni, (90), baada ya kupiga frii-kiki iliyozama moja kwa moja langoni na mechi kumalizika kwa sare ya 1-1.

Taarifa kutoka kambini kwa Simba ilizozipata gazeti hili ni kwamba, kocha Benchikha amefurahia upigaji frii-kiki wa Chama na sasa amewaambia wote (Chama na Saido), kuwa na mawasiliano mazuri na inapopatikana apige mtu atakayekuwa upande sahihi.

"Hata kocha aliwaambia, kwa sasa faulo watakuwa wanapiga wote, uzuri wanaelewana na ni marafiki hivyo ambaye ataona mpira upo upande wake na anaweza kufanya vizuri basi atapiga na mwenzake atafanya jukumu lingine," alisema moja ya wachezaji wa Simba.

Kwa upande wa kocha msaidizi wa timu hiyo, Seleman Matola alisema mchezaji yeyote anayepata nafasi ya kufanya jambo ndani ya Simba anatakiwa kulifanya kwa ustadi, ubora na umakini mkubwa ili kuipatia Simba matokeo chanya.

"Tunacheza kama timu, kila mmoja anafanya jambo kwa ajili ya nembo ya klabu hivyo anayepata nafasi anatakiwa kuitumia vyema," alisema Matola.

Ukiachana na frii-kiki, Saido pia amebaki kuwa na kitengo maalumu cha kupiga penalti za Simba pale itakapopatikana akiwa uwanjani huku Chama naye akiwa na kitengo cha kupiga kona.

Chama hadi sasa amehusika kwenye mabao sita katika ligi, akifunga matatu na kutoa asisti tatu huku Saido akiwa amehusika katika mabao matano, akifunga yote.


ONANA AONGEZA MZUKA
Winga Mcameroon, Willy Onana baada ya kutoonekana kwenye mechi tatu za ligi ilizocheza timu yake, sasa amerejea na huenda akawa sehemu ya kikosi kitakachoivaa Geita Gold, kesho kuanzia saa 10:00 jioni uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mara ya mwisho kwa Onana kuonekana kwenye kikosi cha Simba ilikuwa kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mlandege uliomalizika wa Simba kupoteza 1-0.

Akizungumza na gazeti hili, Onana alisema yupo tayari kwa mchezo na sasa analisikilizia benchi la ufundi tu.
"Nilikuwa na maumivu kidogo lakini sasa niko sawa, nafanya mazoezi na timu na bechi la ufundi ndilo litaamua linanipanga lini," alisema Onana.

Staa huyo aliyetua Msimbazi mwanzoni mwa msimu huu akitokea Rayon Sports ya Rwanda alianza maisha ndani ya Simba kwa kishindo baada ya kufunga bao la kideoni kwenye mechi yake ya kwanza iliyokuwa ya tamasha la 'Simba Day', dhidi ya Power Dynamos kutoka Zambia lakini baada ya hapo alionekana kupoa hadi pale alipoibuka katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca na kufunga mabao mawili yaliyoipa Simba ushindi wa 2-0, mchezo uliopigwa dimba la Benjamin Mkapa Desemba 19, mwaka jana.


MHILU APIGA MKWARA
Nyota wa zamani wa Simba, Yusuph Mhilu anayeichezea Geita Gold ameweka wazi shauku kubwa aliyokuwa nayo ya kupambana na waajiri wake wa zamani.

"Kama ikitokea nimefunga nitashangalia tu kwa sababu Simba tumeshamalizana na nilipita kama timu zingine nilizopitia na nikiifungia nitakuwa na furaha, nawaomba mashabiki wetu waje kwa wingi ili kutoa sapoti ya kutosha kwetu," alisema.

Mhilu alijiunga na Geita dirisha kubwa msimu huu akitokea Kagera Sugar alikopelekwa kwa mkopo wa mwaka mmoja na Simba, aliyojiunga nao Agosti 4, 2021 na kudumu kwa msimu mmoja tu kutokana na kutokuwa katika kiwango bora alichotegemewa.


REKODI ZAIKATAA GEITA
Tangu Geita Gold ipande rasmi Ligi Kuu Bara msimu wa 2020/2021, imekutana na Simba mara nne na kati ya hizo haijawahi kushinda.

Katika michezo hiyo minne, Geita imefungwa mitatu na kutoka sare mmoja tu wa bao 1-1 Mei 22, 2022 huku ikiruhusu mabao 11 na kufunga mawili.
Mchezo wa mwisho uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba baina ya timu hizo Simba ilishinda mabao 5-0, Desemba 18, 2022.