Chama la Wana latenga mzigo bara

Muktasari:
- Chama hilo la Shinyanga lililowahi kutamba Ligi Kuu misimu mitano nyuma, lilimaliza nafasi ya tatu katika Ligi ya Championship msimu huu na kuibuka mshindi wa mechi ya mwisho ya mchujo dhidi ya Geita Gold kwa jumla ya mabao 4-2 na sasa linasubiri kuvaana na timu ya Ligi Kuu.
STAND United ‘Chama la Wana’ imesema baada ya kupenya katika mtoano (play off), ili kupanda Ligi Kuu Bara, kwa sasa ipo tayari kukutana na timu yoyote huku ikitangaza dau nono kwa wachezaji wa timu hiyo iwapo watafanikiwa kuirejesha kwenye ligi hiyo.
Chama hilo la Shinyanga lililowahi kutamba Ligi Kuu misimu mitano nyuma, lilimaliza nafasi ya tatu katika Ligi ya Championship msimu huu na kuibuka mshindi wa mechi ya mwisho ya mchujo dhidi ya Geita Gold kwa jumla ya mabao 4-2 na sasa linasubiri kuvaana na timu ya Ligi Kuu.
Kwa sasa timu hiyo yenye mashabiki na mzuka mwingi mjini humo inasubiri timu itakayopenya kwa zile za Ligi Kuu inyotarajiwa kuzikutanisha itakayomaliza nafasi ya 13 na 14 na itakayopoteza ndio itakayoumana na Stand ili kupigana ibake au iipishe iungane na Mtibwa Sugar na Mbeya City zilizopanda daraja moja kwa moja.
Hata hivyo, hadi sasa timu nane za Ligi Kuu kuanzia Dodoma Jiji iliyopo nafasi ya nane kwa pointi 34 inaweza kuangukia mchujo na kukutana na Stand United katika hesabu za kubaki au kushuka daraja.
Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Fred Masai alisema hadi sasa hesabu zao zimeenda vizuri ambapo wanajipanga kwa ajili ya kukutana na yeyote ili kutimiza ndoto kurejea Ligi Kuu.
Masai alisema baada ya mchezo wa majuzi dhidi ya Geita Gold wametoa mapumziko mafupi ya siku 10 ili wachezaji kutuliza presha kisha kurejea kambini kujiwinda na ngwe ya lalasalama.
“Yeyote atakayekuja mbele yetu ni halali yetu. Tunatarajia baada ya siku 10 timu itarejea tena kambini kusubiri mpinzani yeyote atakayekuja. Kimsingi uongozi umejipanga ndani na nje ya uwanja,” alisema Masai na kuongeza:
“Tukiwa mechi za mwisho Championship bonasi ilikuwa kuanzia Sh1 milioni hadi Sh3 milioni mechi dhidi ya Geita, sasa hapo tutafanya mara mbili yake tunapokwenda kwenye hatua hiyo.”
Kigogo huyo aliongeza kuwa wanafahamu kukutana na timu za Ligi Kuu inakuwa siyo jambo jepesi, lakini kama walivyoazimia kupanda Ligi Kuu msimu ujao haijalishi wanakutana na nani ilmradi watimize ndoto yao.
“Wakati tunaendelea na maandalizi makubwa tutafuatilia timu moja moja kwenye zile zilizo kwenye presha ya play off ili tuwasome mapema kabla ya kukutana nao,” alisema Masai.