Chafua chafua yatetema

Muktasari:

Klabu ya Majeshi ilikuwa ya pili kwa alama 20 ikifuatiwa na Mombasa kwa alama nne kisha klabu za Kentrack na Kibra katika nafasi ya nne kwa alama tatu kila moja.

Mombasa. HAPA ni nomaree, ngumi jiwe tu!  Mabingwa wa ndondi nchini Kenya Polisi almaarufu ‘Chafua Chafua’ walidhihirisha kuwa moto wa kuotea mbali  katika mashindano ya Ligi Kuu nchini.

Stori iko hivi! Kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu mashabiki wa ndondi nchini walipata fursa kushuhudia mapigano ya Ligi Kuu yanayoshirikisha klabu mbili hasimu, Majeshi (KDF) na Polisi katika Uwanja wa Mbuzi, Kongowea.

Klabu hizi mbili zimekuwa zikihepana katika mashindano haya, lakini baada ya kuchaguliwa kwa bosi mpya wa ndondi nchini Anthony Otieno Ombok, zilikubali kwa kauli moja kukabiliana ana kwa ana.

Lakini mwisho wa siku, mashabiki walibaini mbivu na mbichi baada ya Polisi kuibuka kidedea kwa kuzoa jumla ya alama 22 .

Klabu ya Majeshi ilikuwa ya pili kwa alama 20 ikifuatiwa na Mombasa kwa alama nne kisha klabu za Kentrack na Kibra katika nafasi ya nne kwa alama tatu kila moja.

Klabu za Vihiga, Githurai 44 na Nairobi zilipata alama mbili wakati Siaya, Dallas, Magereza, Busia na Laikipia zikitoka na alama moja kila mmoja.

ZANA HATARI

Baada ya kutunishiana misuli kwa muda mrefu, klabu za Polisi na Majeshi ziliamua kuchomoa zana hatari kwa mapambano haya.

Kila mmoja akiingiza maboksa saba katika fainali angalau kuibuka mshindi katika makabiliano haya yaliyoshuhudiwa na idadi kubwa ya mashabiki.

Hivi ndivyo mambo yalivvyokuwa katika Uwanja wa Mbuzi, Kongowea katika makabiliano haya ya mkondo wa tatu wa Ligi Kuu nchini.

 

LIGHT FLY;

Abednego Kyallo wa Majeshi alitumia kila mbinu kabla ya kuibuka mshindi dhidi ya Martin Maina wa Polisi aliyejikaza kisabuni katika raundi zote tatu.

Katika mapigano yao ya nusu fainali, Kyallo alimkung’uta Francis Gitonga wa Laikipia huku Maina akimnyuka Joshua Maina wa Kibra.

 

FLY (52KG)

Mwamba wa timu ya taifa, Shaffi Bakari wa Polisi alipata ushindi wa ubwete baada ya mpinzani wake George Kahindi  wa Mombasa kuingia mitini. Katika pigano lake la nusu fainali, Shaffi alipata kibarua kizito kutoka kwa Thomas Kazungu wa Siaya. Shaffi alimshinda Michael Donga wa Kentrack katika nusu fainali.

 

BANTAM (56KG)

Katika uzani huu, Martin Oduor wa Polisi aliyewahi kuwakilisha taifa mara kadhaa kimataifa alikumbana na kizingiti kigumu mbele ya Denis Muthama wa Majeshi kabla ya kutawazwa mshindi kwa wingi wa alama.

Oduor alimcharaza Cyrus Wandera wa Busia huku Muthama akimshinda Mohammed Ali wa Mombasa katika mapigano ya nusu fainali.

 

LIGHT (60KG)

Boksa Ethan Maina wa Polisi alitumia dakika mbili pekee kumfagilia mbali John Mwanzia wa Githurai 44 kwa njia ya knock-out.

Hadi akitinga fainali, Maina alikuwa kamnyamazisha bingwa wa uzani huo, Nick Okoth wa Majeshi kwa wingi wa alama katika pigano ambalo wengi waliamini Okoth alinyang’anywa ushindi peupe na waamuzi.

 

LIGHTWELTER (64KG)

Ijapo Stanley Ogutu wa Kentrack alisalimu amri mikononi mwa binga Victor Odhiambo wa Majeshi lakini alipigana kiume katika raundi zote tatu.

Kukosa kusiriki kwa Isaya Odhiambo wa klabu ya Kongowea katika mashindano haya kulimpatia Victor mwanya wa kutamba katika uzani huu.

 

WELTER (69KG)

Boniface Mogunde wa Polisi aliibuka mshindi katika uzito huu baada ya kumshinda Chris Muremi wa Majeshi katika pigano iliyokuwa na makabiliano makali.

Katika pigano lake la nusu fainali Mogunde alimshinda Moses Biko wa Vihiga wakati Muremi akimshinda Denis Ngesa wa Siaya.

 

MIDDLE (75KG)

Kinyume na matarajio ya wengi, chipukizi George Ouma wa Polisi aliwashangaza wengi alipompiga intanashenali Edwin Okong’o wa Majeshi kwa wingi wa alama.

Kabla ya kutinga fainali, Ouma alimshinda Benjamin Asikoyo wa Vihiga huku Okong’o akimnyanyasa Chrispin Ochanda wa Nairobi.

 

LIGHTHEAVY (81KG)

Hezron Maganga wa Majeshi aliwafurahisha mashabiki kwa kumcharaza intanashenali Humphrey Ochieng’ wa Polisi kama gunia la kufanyia mazoezi katika raundi zote tatu.

Maganga alimshinda Joseph Odhiambo wa Magereza katika nusu fainali wakati Ochieng’ akimkung’uta Gently Omondi wa Busia.

HEAVY (91KG)

Bingwa wa taifa Elly Ajowi wa Polisi kawa na kazi wastani kumkung’uta George Wenjuli wa Busia aliyeonekana kupepesuka kila mara jukwaani.

SUPERHEAVY (91+ KG)

Fredrick Ramogi aliandikisha ushindi wa cheee baada ya mpinzani wake Alamin Somo wa Mombasa kuingia tumbo joto na kisha kuingia mitini. Katika nusu fainali Ramogi alimshinda James Mahiu wa Nairobi.

Katika mapigano ya akina dada mambo yaliwa hivi;

LIGHTFLY (48KG)

Bingwa wa taifa Christine Ongare wa Polisi alikosa mpinzani hivyo kupata ushindi bila jasho.

FLY (51KG)

Bingwa Veronica Mbithe wa Majeshi alilazimika kutumia kila mbinu kabla ya kupata ushindi wa chupuchupu dhidi ya Flavian Auma wa Busia .

BANTAM (54KG)

Pauline Chege wa Nanyuki alimshinda Alice Waiyego wa Nairobi kwa wingi wa alama.

LIGHT (60KG)

Beatrice Akoth wa Nairobi alimduwaza bingwa Teresia Wanjiru wa Magereza kwa wingi wa alama katika pigano lililowaacha mashabiki kwa mashangao mkubwa.

LIGHTWELTER (64KG)

Everlyn Akinyi wa Kisumu alitumia dakika moja pekee kumkomoa Sharon Nyongesa wa Trans Nzoia aliyeshindwa kujitetea vilivyo mara baada ya kengele ya pigano kulia.

WELTER (69KG)

Bingwa Lorna Kusa alimkung’uta Maurine Nabwire wa Busia kwa njia ya knock out katika raundi ya pili katika pigano lililotarajiwa kumaliza raundi zote tatu.

MIDDLE (78KG)

Elizabeth Andiego boksa wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kushiriki michezo ya Olimpiki alihihirisha kuwa moto wa kuotea mbali kwa kumshinda Lilian Achieng’ wa Nairobi kwa alama nyingi.

HEAVY (81 KG)

Boksa huyu wa klabu ya Polisi  anayeinukia kwa kasi Elizabeth Akinyi aliandikisha ushindi wa bwerere baada ya kukosa mpinzani katika mashindano haya.