Cedric Kaze, Ntibazonkiza wanatupigia kengele masikioni

ERASTO Edward Nyoni aliacha jina kubwa Burundi. Pengine ndiye mchezaji wa Kitanzania aliyecheza kwa mafanikio zaidi Burundi. Alikuwa katika klabu ya Vital’O. Baadaye aliamua kurudi nyumbani. Alirudi zake na mke wa Kirundi ambaye alidumisha utawala wa Warundi waliowahi na wanaotesa nchini. Ndiyo, Warundi wametutesa mwanzo na mpaka sasa. Ndani na nje ya uwanja. Zamani Simba waliwahi kuwa na kipa wa Kirundi aliyeitwa Mckenzie Ramadhan. Lakini Yanga waliwahi kuwa na kocha wa Kirundi, Nzoyisaba Tauzany.

Na miaka ya karibuni wamekuwepo wachezaji wengi wa Kirundi waliotesa Tanzania wakiongozwa na Amiss Tambwe ambaye ameacha jina kubwa nchini. Walikuwepo pia akina Laudit Mavugo na wengineo lakini Tambwe aliacha jina kubwa zaidi.

Upande wa makocha wamerudi tena kwa kasi. Kitu kizuri zaidi wanastahili. Kocha wetu wa timu ya taifa, Ettiene Ndayiragije ni Mrundi. Kocha wa Namungo, Itimana Thierry ni Mrundi. Kocha aliyepita wa KMC, Haruna Harerimana ni Mrundi.

Na sasa mkononi mwetu amewasili kocha, Cedric Kaze kutoka Burundi. Huyu amejikuta akiambatana bila ya kutarajia na mshambuliaji wa Kiburundi, Said Ntibazonkiza ambaye alichukuliwa hivi karibuni na Yanga baada ya kuona uwezo wake katika pambano kati ya Taifa Stars dhidi ya Burundi.

Tuanze kwa wachezaji. inachekesha kidogo wakati wachezaji kutoka katika nchi yenye wakazi 11 milioni wakivamia katika nchi yenye wakazi 56 milioni. Hesabu rahisi za maisha ya mwanadamu huwa zinakataa. Wengi inabidi waende katika upande wa walio wachache. Ukanda huu wachache wanavamia kwenda upande wa walio wengi.

Kwa mfano, nchi za Nigeria na Brazil zinatoa wachezaji wengi duniani kwa sababu wana idadi kubwa ya watu. Ghafla timu zinakuwa chache kuliko mahitaji ya wachezaji. Tanzania na Burundi hali ni tofauti. Wachache wanakwenda upande wa walio wengi.

Zitatajwa sababu nyingi. Ya kwanza tutaambiwa kwamba mpira wa Burundi haulipi sana kama wa Tanzania. Sijui. Inawezekana ni kweli lakini wachezaji wa nchi kama hizi za Nigeria na Brazil huwa wanakwenda katika nchi ndogo za kawaida kwa ajili ya kutafuta namna ya kupenya na kuvuka kuelekea kwingineko.

Labda inawezekana wachezaji wetu hawana kiu sana lakini ingekuwa nchi nyingine bado wangetumia umaskini huo huo wa Burundi kwa ajili ya kujenga majina yao na kuhakikisha wanakwenda mbali zaidi. Haishangazi kuona kuna Wanigeria na Wabrazil kibao wanacheza soka Macedonia.

Kuna nchi zenye raia wengi kama China na India ambazo unaweza kuzipa msamaha kwa sababu soka sio mchezo unaopendwa zaidi katika nchi hizo. Lakini kwa Tanzania hauwezi kutoa msamaha pale tunaposhindwa kupeleka wachezaji wengi nje kuliko wageni wanaoingia. Kuna mahala kiu imekosekana au mipango imekosekana.

Tugeukie upande wa makocha. Hapa kuna shida zaidi. Licha ya idadi ndogo ya watu lakini Waburundi wamekuja kutufundisha mpira. Kaze amekuja kufundisha moja kati ya klabu kubwa nchini. Yanga. Usichukulie kwa urahisi hasa katika nyakati hizi ambazo klabu hizi zinafundishwa na wazungu.

Kabla yake, Ndayiragije aliwahi kufundisha klabu ya Mbao, kisha akaenda klabu kubwa nchini Azam halafu akaibukia timu ya taifa. Kifupi Kaze anafundisha Yanga, wakati Ndayiragije alifundisha Azam. wameaminiwa nini katika kipindi hiki ambacho viongozi na mashabiki wanaamini zaidi makocha Wazungu? Sio bure kwamba makocha hawa wapo nchini. Wana wasifu (CV) za kutosha kuwepo hapa. Warundi wamekuwa wakizalisha makocha wengi vijana katika miaka ya karibuni. Wana programu maalumu kwa ajili ya kuzalisha makocha.

Hawa akina Kaze na Ndayiragije wamesomea nje ya nchi yao. Huwa wanakwenda Ufaransa, Ubelgiji, Hispania na kwingineko kwa ajili ya kusomea ukocha katika ngazi za juu. Sisi hatuna makocha kama hawa katika miaka ya karibuni. Tangu Charles Boniface Mkwassa aende kusomea Ujerumani sijasikia makocha wengine wakienda kusomea.

Kwanini? Nadhani hatuna watu waliopania kuwa makocha katika ngazi za juu. Zamani walikuwa wanadai wanabaniwa lakini kila siku ukweli unajiweka wazi. Lnasemekana lugha ni kikwazo pia lakini vyovyote ilivyo inaonekana ukocha sio shughuli yetu tena. Makocha wetu wapo tayari kuwa wasaidizi kwa wazungu au kwa hawa akina Kaze. Makocha wetu huwa wanajinasibu kuwa na kazi zao nyingine nje ya mpira ambazo zinawapatia vipato. Hili huwa wanalisema bila ya aibu. Hapa wanakuwa wanatuthibitishia kwamba mpira sio kazi yao.

Hawa makocha wa Kirundi hawana kazi nyingine zaidi ya mpira. Wamejikita katika mpira. Wamewekeza nguvu na akili zao katika mpira. Tazama njia ambayo Ettiene amepitia. Jinsi alivyokubali kwenda katika timu kama Mbao ya Mwanza akaisuka. Akaonwa na Azam. akafanya kazi nzuri akaenda timu ya taifa.

Mpira unabadilika kila kukicha na ni wazi kwamba makocha wetu inabidi warudi shule mara kwa mara. Ukikaa na Ettiene unaona wazi ni mtu anayeufahamu mpira. Ukikaa na Thierry wa Namungo unaona wazi kwamba ni mtu anayeufahamu mpira.

Nimemsikiliza Kaze katika mahojiano yake ya kwanza nchini anaonekana ni mtu ambaye anaufahamu mpira. Anaweza kufaulu au kufeli lakini ukimsikiliza tu unajua kwamba anaufahamu mpira. Anaweza asiwe mtu mzuri katika kufikisha mawazo yake kwa wachezaji lakini anaufahamu mpira.